IQNA

Mahakama Nigeria yapongezwa na Waislamu kwa kuondoa marufuku ya Hijabu

0:04 - July 25, 2016
Habari ID: 3470472
Waislamu nchini Nigeria wamepongeza hukumu ya Mahakama ya Rufaa mjini Lagos kubatilisha marufuku ya wasichana Waislamu kuvaa Hijabu katika shule za serikali mjini humo.

Shirika moja la kutetea haki za Waislamu nchini humo linaloitwa Muslim Rights Concern (MRC) limeipongeza Mahakama ya Rufaa kwa kufuta marufuku hiyo na kusisitiza kuwa, uamuzi huo ni ushindi kwa jamii ya Waislamu nchini. Jaji wa mahakama hiyo alisema kuwazuia mabinti wa Kiislamu kuvaa vazi hilo la stara kwa mujibu wa mafundisho ya dini yao eti kwa kigezo kuwa hakuendani na kanuni za shule, ni kukiuka katiba ya nchi inayosisitiza kuwa, kila mmoja ana haki ya kuabudu na kufuata maelekezo ya imani yake madhali maelekezo yale hayakiuki haki za wengine. Haijabainika iwapo serikali ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika itaelekea katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi huo wa Mahakama ya Rufaa.

Mapema mwaka huu, jumuiya za Kaislamu nchini Nigeria zilitoa taarifa ya kulaani vikali azma ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo ya kutaka kupiga marufuku vazi la hijabu na kusema kuwa, sera kama hiyo ni njia ya kukwepa utatuzi wa matatizo ya kimsingi ya nchi hiyo. Aidha Jumuiya ya Mawakili Nigeria (NBA) ilisema kupigwa marufuku vazi la kujisitiri wanawake Waislamu yaani hijabu ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.

Kauli hizo zilitolewa baada ya Buhari kusema kuwa baadhi ya wanaotekeleza hujuma za kigaidi nchini ni wanawake wanaovaa hijabu na kwamba iwapo italazimu, serikali yake haitakuawa na njia nyingine ghairi ya kuchagua moja kati ya mambo mawili ima vazi la hilo la staha au usalama wa taifa.

Waislamu wanakadiriwa kuwa asilimia 70 ya wakaazi wote milioni 173 katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

3460464

captcha