IQNA

17:37 - February 05, 2021
Habari ID: 3473624
TEHRAN (IQNA) Wanawake Waislamu nchini Nigeria wamemtaka rais wa nchi hiyo Muhammadu Buhari na magavana wa majimbo watunge sheria za kuwaadhibu wale wanaowabagua wanawake Waislamu kwa sababu tu wamevaa Hijabu.

Katika kikao kilichoitishwa na jumuia mbali mbali za Kiislamu mjini Lagos, kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Hijabu Februari Mosi, washiriki walilaani vikali wanaowasumbua na kuwakera wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu.

Washiriki wa kikao hicho walisema Kamisheni ya Kitaifa ya Vitambulisho na Tume ya Kitaifa ya Mitihani, shule na taasisi binafsi ni miongoni mwa wahusika wakuu katika kuwasumbua wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu.

Akizungumza katika kikao hicho, Hajia Mutiat Orolu-Balogun wa Jumuiya ya Kutetea Haki za Kuvaa Hijabu ameitaka serikali ya Nigeria ihakikishe kuwa wale wanaowabagua wanawake Waislamu kwa sababu tu wanavaa Hijabu wachukuliwe hatua za kisheria. Amesema wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu wananyimwa huduma za vitambulisho, na pia wengine wanazuiwa kushiriki katika mitihani ya kitaifa na hata baadhi wanazuiwa kuingia katika benki ambazo ziko katika majengo yanayomilikiwa na makanisa.

Naye Amirah Hajja Hafsat Shidi mwakilishi wa Baraza la Kitaifa la Jumuiya za Vijana Waislamu Nigeria katika jimbo la Lagos ametoa wito kwa jamii kukabiliana na kile alichokitaja kuwa ni 'chuki dhidi ya Hijabu' au Hijabophobia. Amesema chuki hiyo ina taathria hasi kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Waislamu wanakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu wote takribani milioni 200 nchini Nigeria.

3952169/

Kishikizo: waislamu ، nigeria ، wanawake ، Hijabu
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: