IQNA

Mwanazuoni wa Nigeria katika mzungumzo na IQNA:

Serikali ya Nigeria yaweka vizingiti katika maadhimisho ya Siku ya Ashura

13:17 - October 05, 2016
Habari ID: 3470600
Pamoja na kuwa serikali ya Nigeria kidhahiri imetangaza Waislamu wa madhehebu ya Shia hawatawekewa vizingit katika maombolezo ya siku 10 za Muharram, imebainika kuwa kuna vizingiti katika Siku ya Ashura.

Katika mahojiano maalumu na IQNA, Sheikh Salim Mohammad Sani, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Rasul al Aadham SAW Nigeria, amesema serikali ya Nigeria kidhahiri haipingi maombolezo ya Mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS. katika Misikiti na Husseiniya (kumbi za kidini) lakini imebainika kuwa wale wote wanaotaka kufanya maombolezo Siku ya Ashura nje ya Misikiti wanapaswa kupata kibali rasmi cha serikali.

Ameongeza kuwa: "Pengine iwapo kutakuwepo kibali rasmi cha Siku ya Ashura, na kuwepo nidhamu maalumu katika maombolezo, hakutajiri tatizo."

Sheikh Salim Mohammad Sani ameashiria hali ya Mashia nchini Nigeria na kusema: "Mashia nchini Nigeria wana taasisi mbali mbali ikiwemo Harakati ya Kiislamu Nigeria, INM, inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky ambayo pia inajuhisisha na masuala ya kisiasa. Hatahivyo kuna taasisi zingine kadhaa za Kishia ambazo zinajihusisha tu na masuala ya kidini na kiutamaduni."

Sheikh Sani amesema Taasisi ya Rasul al Aadham SAW Nigeria ina makao yake huko Kano kaskazini mwa nchi hiyo na kuongeza kuwa: "Taasisi hii hadi sasa imejenga na kuanzisha misikiti na vituo vya kidini katika maeneo mbali mbali Nigeria."

Ikumbukwe kuwa kati ya Desemba 12-14 mwaka 2015, Jeshi la Nigeria liliwashambulia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria IMN katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Jeshi lilidai kuwa wafuasi wa IMN walikuwa na jama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria hata hivyo inasisitiza kuwa zaidi ya Waislamu 1000 waliuliwa na jeshi la nchi hiyo katika hujuma hiyo.

Aidha Jeshi la Nigeria lilimkamata Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria akiwa pamoja na mke wake. Hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky inaripotiwa kuwa mbaya huku taarifa zikisema amepoteza jicho moja mbali na majeraha mengine mwilini. Serikali ya Nigeria inamshikilia kiongozi huyo wa Kiislamu tokea Desemba mwaka jana pasina kumfungulia mashtaka.

Kuhusiana na tukio la Ashura, miaka 1377 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi katika siku hiyo ya Ashura.

3535520


captcha