IQNA

Kadhia ya Palestina

Ayatullah Khamenei aonana na Sheikh Zakzaky, asema Palestina ni dhihirisho la nguvu za Uislamu

19:01 - October 15, 2023
Habari ID: 3477740
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonana na Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na kusisitiza kuwa, Palestina na Ghaza ni dhihirisho la nguvu za Uislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Jumamosi asubuhi ameonana na Sheikh Ibarahim Zakzaky, Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria hapa mjini Tehran na huku akimpongeza kwa jitihada na kujitolea kwake kikamilifu katika kuupigania Uislamu nchini Nigeria amesema, nguvu za Uislamu zinazidi kuongezeka licha ya kuweko njama kubwa na za kila namna za maadui. Ameongeza kuwa, leo hii moja ya madhihirisho ya nguvu za Uislamu ni haya masuala yanayoendelea hivi sasa  huko Palestina.

Amesema, matukio ya hivi sasa ya Palestina hasa jinai za Wazayuni za kuwashambulia kwa mabomu na kuwaua shahidi wanawake, watoto wadogo na wanaume wasio na hatia zinamsikitisha kila mtu; lakini katika upande mwingine, matukio hayo yanaonesha nguvu za kupigiwa mfano za Uislamu na kwa uwezo na taufiki ya Allah Mtukufu, harakati hiyo iliyoanza huko Palestina itaendelea na itaishia kwenye ushindi kamili wa Wapalestina.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, watu wote katika Ulimwengu wa Kiislamu  wana jukumu la kuwasaidia wananchi wa Palestina.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei vilevile amesema, kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran na serikali iliyojengwa juu ya msingi wa fikra ya Uislamu wa kisiasa baada ya kupita karne nyingi, ni mfano mwingine wa nguvu za Uislamu.

Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu ilipoanzishwa hadi hivi sasa inazidi kuwa imara, nguvu zake zinaongezeka siku baada ya siku na katika siku za usoni pia itazidi kuwa imara na yenye nguvu kubwa zaidi.

Ameongeza kuwa, harakati za Kiislamu duniani zinazidi kuongezeka siku baada ya siku na kusisitiza kuwa: Hivi sasa kuna harakati mbalimbali za Kisilamu katika kona zote za dunia kama za Afrika, Asia, Ulaya na kaskazini mwa bara la Amerika; na kwa uwezo na taufiki ya Mwenyezi Mungu, harakati hizo zitaendelea kwa nguvu kubwa zaidi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea pia kufurahishwa na mazungumzo yake hayo na Sheikh Zakzaky na kuonana kwake na familia ya mwanachuoni huyo mkubwa wa nchini Nigeria.

Kwa upande wake, Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema kuwa, yeye na familia yake wanamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa ya kuonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na hawana maneno ya kuelezea furaha yao. Amemkhutubu Kiongozi Muadhamu akimwambia: Ni matumaini yangu dua zako na jitihada za Waislamu zitaufanya Uislamu uzidi kuimarika na kuwa na nguvu duniani.

3485573

Habari zinazohusiana
captcha