IQNA

UN: Mateso ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar ni zaidi ya inavyodhaniwa

17:59 - February 28, 2017
Habari ID: 3470871
IQNA-Umoja wa Mataifa umesema ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wa Myanmar umefikia kiwango cha kutia wasi wasi na ni mkubwa zaidi ya ilivyodhaniwa.

Mapema mwezi huu, ripoti ya Umoja wa Mataifa ilivitaka vikosi vya usalama vya Myanmar vikomeshe jinai zake dhidi ya Waislamu wa Rohingya yakiwemo mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu hao.

Ripoti hiyo ya UN ilisema kuwa, mbali na mauaji na vitendo vya utumiaji mabavu vya vikosi vya usalama vya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya, vikosi hivyo vimefanya vitendo vya ubakaji, mateso na hata kuwatishia kwa silaha Waislamu wa jamii hiyo sambamba na kuwaua watoto wao.

Mabudha wenye misimamo ya kurufutu ada wamekuwa wakishirikiana na maafisa usalama wa Myanmar katika mauaji na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya katika mkoa wa Rakhine kwa muda sasa, huku hujuma hizo zikishadidi tokea mwaka 2012.UN: Mateso ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar ni zaidi ya inavyodhaniwa

Yanghee Lee, Mjumbe Maalumu (Rapporteur Special) wa UN aliyetumwa kuwatembelea Waislamu wa Rohingya waliokimbilia Bangladesh amesema simulizi alizopewa na wakimbizi hao wa Myanmar ni za kuhuzunisha na zinazoashiria ukubwa wa jinai za kutisha wanazofanyiwa wenzao waliobaki Myanmar.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, wanawake Waislamu wa Rohingya wamemueleza jinsi wenzao walivyobakwa kwa umati na maafisa usalama wa Myanmar, baadhi yao wakichinjwa huku watoto wakitupwa kwenye moto mkali wakiwa hai. 

Hivi karibuni pia,  Zeid bin Ra’ad al-Hussein Kamishna wa Haki za Binadamu aktika Umoja wa Mataifa amesema vikosi vya usalama Myanmar vimetekeleza mauaji ya umati, ubakaji wa Waislamu kigenge na kuteketezwa vijiji vyao katika kampeni mpya ya ukandamizaji iliyoanza mwezi Okotba mwaka jana .

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu hao ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.


3462308

captcha