IQNA

Waislamu Tanzania wasisitiza umoja kuhusu mwezi mwandamo

19:47 - May 27, 2017
Habari ID: 3470996
TEHRAN (IQNA)-Maulamaa wa Kiislamu nchini Tanzania wamesisitiza kuhusu kuhifadhi umoja wa wa Waislamu katika suala la mwezi mwandamo na kutangaza kuanza na kumalizika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, hayo yamesemwa katika mkutano uliofanyika Ijumaa 26 Mei 2017 mjini Dar es Salaam. Kikao hicho cha viongozi na shakhsia mbali mbali wa kidini na kisiasa kilihudhuriwa na Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakr Zuberi, Ali Hassan Mwinyi Rais wa Pili wa Tanzania nakuanzia 1985 hadi 1995 ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 90, Dkt. Gharib Bilal Makamu wa Zamani wa Rais wa Tanzania na mabalozi wa nchi kadhaa za Kiislamu akiwemo balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania.

Katika kikao hicho, Sheikh Abubakr Zuberi, Dkt. Gharib Bilal na Ali Hassan Mwinyi walizungumza na kusisitiza ulazima wa umoja wa Waislamu katika suala la mwezi mwandamo na kuanza na kumalizika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Wazungumzaji aidha walisisitiza kuwa umoja wa Uislamu ni katika dharura za zama hizi na kuongeza kuwa kuwepo hitilafu katika fatawa za madhehebu mbali mbali za Kiislamu ni jambo la kawaida. Kwa msingi huo wamesisitiza kuwa, suala hilo halipaswi kukuzwa na kuwa chanzo cha kuzozana, kutengana na kukufurishana katika umma wa Waislamu.

Inafaa kuashiria hapa kuwa Waislamu wa Tanzania na Kenya leo Jumamosi 27 Mei wamejiunga na aghalabu ya Waislamu duniani kuanza saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani baada ya kuripotiwa kuandama mwezi katika mwambao wa Afrika Mashariki.

3603719


captcha