IQNA

10:17 - May 17, 2018
News ID: 3471516
TEHRAN (IQNA)- Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamewatumia Waislamu na viongozi wa nchi za Kiislamu duniani salamu za kheri na fanaka kwa munasaba wa kuwadia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Katika aghalabu ya nchi za Kiislamu, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Alkhamisi Tarehe 17 Mei 2018 imetangazwa kuwa ni siku ya kwanza ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Rais Hassan Rouhan wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewatumia ujumbe tofauti wa salamu za Ramadhan viongozi wa nchi za Kiislamu duniani.

Katika ujumbe wake, Rais Rouhani amesema kuwa leo hii nafasi ya viongozi wa nchi za Kiislamu ni muhimu sana kuliko wakati mwingine wowote ule katika kulinda utambulisho wa Kiislamu, kujiweka mbali na misimamo mikali na kuwa na misimamo ya pamoja katika kupambana na machafuko na kukabiliana na siasa za kiistikbari na mabeberu wa dunia, na pia katika kufanikisha jitihada za kuleta amani, uadilifu na utulivu kwa wanadamu wote duniani na hasa Waislamu.

Aidha Rais Rouhani ameelezea matumaini yake kwamba kwa kuanza mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, wanadamu wote watapata uhai mpya wa kuwa watu wema, wenye fikra na wenye mfungamano wa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Halikadhalika Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaombea taufiki, mafanikio, ustawi, ufanisi na furaha tele Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu wa kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kwa upande wake, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Ali Larijani amewatumia maspika wa mabunge ya nchi za Kiislamu salamu kwa mnasaba wa kuwadia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Katika ujumbe wake, Larijani amesema: "Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni fursa nzuri ya kuimarisha mshikamano na umoja miongoni mwa mataifa ya Waislamu na kutatua hitilafu zilizopo katika jamii za Kiislamu."

Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa: "Mshikamano na muungano wa nchi za Kiislamu ni mambo ambayo yataleta usalama na utulivu endelevi katika ulimwengu wa Kiislamu."

Larijani amesisitiza kuwa: "Bunge la Iran linaunga mkono kuimarishwa ushirikiano zaidi miongoni mwa mabunge ya nchi za Kiislamu kwa lengo la kuleta umoja na mshikamano ili hatimaye kuondoa hitilafu na vitisho vilivyopo katika umma wa Kiislamu."

Spika wa Bunge la Iran amewatakia Waislamu wote duniani kheri na  fanaka katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

/3715127

Name:
Email:
* Comment: