IQNA

10:24 - November 07, 2018
News ID: 3471733
TEHRAN (IQNA) - Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad al Mustafa SAW aliaga dunia tarehe 28 Safar mwaka wa 11 Hijiria katika mji mtakatifu wa Madina akiwa na umri wa miaka 63 na kuzikwa katika mji huohuo.

Kwa mujibu wa riwaya nyingi zilizopo, yapata miongo minne baada ya kifo cha Bwana Mtume SAW yaani tarehe 28 Swafar mwaka 50 Hijiria, mjukuu wake mpendwa Imam, Hassan Mujtaba AS naye aliuawa shahidi na vibaraka wa mtawala dhalimu, Muawiyya. Vifo hivyo vya Mtume na mjukuu wake katika nyakati tafauti viliiachia huzuni kubwa jamii ya Kiislamu. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka vifo vya watukufu hawa wawili.

Taa inayoangaza
Katika Aya zake, Qur'ani Tukufu inamtaja Mtume kama taa inayoangaza katika njia ya wokovu wa Mwenyezi Mungu na kwamba ni rehema kwa walimwengu na ruwaza njema kwa wale wanaotaka kuwa na maisha mema humu duniani na huko Akhera. Aya hizo pia zinakumbusha kwamba hata kama Mtume SAW ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu anayewasiliana moja kwa moja na nguvu za mbinguni, lakini wakati huohuo ni mwanadamu kama wanadamu wengine, ambaye anahitajia chakula, mavazi, ndoa, huwa mgonjwa na pia kuzeeka. Hivyo wakati wake ulipowadia, aliitikia wito wa Mwenyezi Mungu kama wanavyofanya wanadamu wengine wote. Katika Hija yake ya mwisho na alipokuwa akimpiga shetani mawe, Mtume Mtukufu (saw) aliwaambia Waislamu: 'Jifundisheni amali za Hija kutoka kwangu kwa sababu baada ya mwaka huu huenda nisifanikiwe tena kuja Hija na huenda hamtaniona tena nikiwa katika nafasi hii.' Mtume SAW alikuwa mgonjwa katika siku za mwisho za maisha yake humu duniani. Akiwa katika hali hiyo ya kuumwa alienda msikitini na baada ya kuswali alisema: 'Enyi watu! Moto mkali wa fitina umewashwa na fitina kuenea kama yanavyoenea mawimbi ya usiku mkubwa. Mimi nitakutangulieni katika siku ya Ufufuo na nyinyi mtafika mbele yangu kwenye Hodhi ya Kauthar. Fahamuni kwamba nitakuulizeni kuhusu Thaqalain (Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlu Beit wangu). Hivyo tazameni mtaamiliana vipi na viwili hivi baada yangu. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu Mrehemevu na anayejua mambo yote amenijulisha ya kwamba viwili hivi havitatengana hadi vitakaponifikia. Jueni kwamba nimekuachieni viwili hivi, hivyo msivitangulie msije mkasambaratika na kugawanyika wala msivipuuze mkaja kuhiliki.' Baada ya hapo Mtume SAW akaanza safari ya kuelekea kwa Muumba wake kwa usumbufu.

'Niitieni ndugu na rafiki yangu'
Watu wakaanza kumuaga Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu huku macho yao yakiwa yamejaa machozi. Hata akiwa katika hali ya maumivu makubwa ya ugonjwa, Mtume aliwausia sana watu wa pembeni yake kuhusu umuhimu wa kushughulikia matatizo na mahitaji ya watu na kuzingatia haki zao. Kisha aliwaambia hadhirina: 'Niitieni ndugu na rafiki yangu.' Ummu Salama, mkewe Mtume SAW akasema: 'Muiteni Ali kwa sababu Mtume hamkusudii mtu mwingine isipokuwa Ali.' Ali alipofika, Mtume alimuashiria amkaribie. Kisha alimkumbatia kwa muda mrefu huku akimnong'oneza na kumwambia siri zake hadi akazimia. Baada ya kuona hali hiyo wajukuu wa Mtume SAW Hassan na Hussein AS walilia sana na kuuangukia mwili wake. Imam Ali AS alitaka kuwatoa juu ya mwili wa Mtume SAW lakini akazinduka ghafla na kusema: 'Eeh Ali! Waache wawili hao nipate kunusa harufu yao nao wanuse harufu yangu, ili wanufaike nami na mimi ninufaike nao.'
Hapo Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu akaaga dunia. Aliaga dunia akiwa mikononi mwa Ali bin Abi Talib AS ambaye aliwatangazia watu waliokuwa karibu kuhusu kifo cha mtukufu huyo SAW . Kifo cha Mtume SAW kilikuwa kichungu na chenye huzini kubwa kwa serikali na umma wa Kiislamu. Katika kipindi kifupi, Mtume Mtukufu SAW alifanikiwa kuanzisha mazingira mazuri ya upendo, udugu na urafiki kati ya watu na kuasisi serikali iliyoeneza uadilifu na uzingatiaji sheria katika jamii, ambapo kila mtu na hasa tabaka la watu wa kawaida walinufaika sana kutokana na hali hiyo.
Hatua alizozichukua Mtume Muhammad SAW katika kipindi cha miaka 23 ya Utume wake, zinachukuliwa kuwa hatua na harakati muhimu zaidi za kihistoria kuwahi kuchukuliwa katika jamii ya mwanadamu. Alianzisha jamii mpya, kuunganisha Bara Arabu katika mfumo wa kisiasa na kijamii juu ya msingi wa Qur'ani na kujaza imani kwenye nyoyo na fikra za wafuasi wake. Wafuasi wake hao walieneza ujumbe huo katika pembe na maeneo ya mbali zaidi duniani. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa taathira ya Mtume Muhammad SAW katika historia ni kubwa zaidi kuliko taathira za watu wengine wote katika historia ya mwanadamu.

Ustaarabu wa Kiislamu
Sifa muhimu ya ustaarabu ulioanzishwa na Mtume SAW ni ya upole na huruma mkabala wa taasubi za kikabila na kidini zilizotawala katika zama hizo. Mtume SAW alichangia na kuimarisha pakubwa elimu, taaluma na sanaa za mwanadamu kwa kuwasilisha njia za wastani na za kati kwa kati katika mienendo na miamala ya watu. Hatua za Mtume SAW katika kuasisi jamii iliyostaarabika na iliyo na serikali kuu yenye taasisi na idara za kisiasa na kisheria zinazoendeshwa kwa msingi wa taratibu zilizo wazi, zilipelekea kubadilishwa mifumo ya jamii za kijahilia. Jambo hilo pia lilipelekea kuanzishwa ustaarabu halisi uliosimama juu ya misingi ya ubunifu na uvumbuzi kwa kadiri kwamba jamii za Kiislamu na zisizo za Kiislamu zingali zinanufaika na matunda ya kimaada na kimaanawi ya uvumbuzi huo hadi leo.
Hata kama Mtume Mtukufu SAW hayuko tena pamoja nasi, lakini ni wazi kwamba ujumbe wake ni uleule ujumbe wa Tauhidi ambao ndio unaoangaza ulimwengu na kuufanya uvutie wanadamu. Huu ndio ujumbe wa kwanza wa Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, kwa maana ya kutotogemea nguvu nyingine yoyote isipokuwa ya Mwenyezi Mungu na vilevile kutokubali aina yoyote ya dhulma na uonevu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 25 ya Surat al-Anbiyaa: Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimpa Wahyi ya kwamba hapana mungu isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.
Tunachukua fursa hii kutoa mkono wa pole kwa Waislamu na wapenda haki kote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka kifo cha Mtume Mtukufu Muhammad SAW na mjukuu wake mwema Imam Hassan AS.

3761831

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: