IQNA

Siku ya Pili ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Saudia

23:27 - August 11, 2025
Habari ID: 3481068
IQNA – Siku ya pili ya Mashindano ya 45 ya Kimataifa ya Mfalme Abdulaziz ya Kuhifadhi, Kusoma kwa Tajwidi na Kufasiri Qur’ani Tukufu ilishuhudia washiriki 17 kutoka pembe mbalimbali za dunia wakisoma mbele ya hadhira katika Msikiti Mtukufu wa Makkah.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Kiislamu, Da‘wah na Mwongozo ya Saudi Arabia, ratiba ya siku hiyo ilijumuisha washiriki wanane katika kikao cha asubuhi na washiriki tisa katika kikao cha jioni, wakiwakilisha makundi yote matano ya mashindano.

Washiriki walitoka Mali, Ethiopia, Kazakhstan, Nigeria, Maldives, Albania, Australia, Misri, Libya, Uzbekistan, Qatar, Kuwait, Hungary, Yemen, Malaysia, na Shirikisho la Urusi.

Mashindano haya, ambayo sasa yako katika toleo lake la 45, yalifunguliwa rasmi Jumamosi katika Msikiti Mtukufu na Waziri wa Mambo ya Kiislamu, Sheikh Abdullatif Al Alsheikh, ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mashindano ya Qur’ani ya kitaifa na kimataifa.

Yakiwa chini ya udhamini wa Mfalme wa Saudi Arabia, hafla hii imevutia washiriki 179 kutoka nchi 128.

Mashindano haya yanatoa jumla ya zawadi ya Riyal za Kisaudia milioni 4, pamoja na zawadi za fedha taslimu kiasi cha Riyal milioni 1 kwa washiriki wote.

Katika siku ya kwanza, jopo la majaji liliwasikiliza washiriki 14 kutoka nchi 13, na kufanya idadi ya waliokwishasailiwa kufikia washiriki 31.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawakilishwa na washiriki wawili: Mehdi Barandeh, anayeshindana katika kundi la kuhifadhi Qur’ani yote, na Seyed Hossein Moqaddam Sadat, anayeshiriki katika kundi la kuhifadhi Juzuu 15.

Mashindano ya Kimataifa ya Mfalme Abdulaziz yanachukuliwa kuwa miongoni mwa mashindano ya heshima na hadhi kubwa zaidi duniani ya Qur’ani, yakivutia wasomaji na wahifadhi bora kutoka ulimwengu mzima wa Kiislamu na kwingineko. Raundi za mwisho zitaendelea katika Msikiti Mtukufu hadi pale washiriki wote watakapomaliza kusikilizwa.

/3494210

captcha