IQNA

Wito wa ushiriki katika Tuzo ya 11 ya Kimataifa ya Arbaeen

23:21 - August 13, 2025
Habari ID: 3481078
IQNA – Mashindano ya 11 ya Kimataifa ya Arbaeen yametangaza rasmi mwaliko wa ushiriki katika nyanja mbalimbali za sanaa na fasihi.

Taasi ya Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu Iran (ICRO) imesambaza video sambamba na tangazo la mwaliko rasmi wa kushiriki katika toleo hili la kumi na moja la Tuzo ya Kimataifa ya Arbaeen.

Kazi zitakazopokelewa zitajumuisha vipengele kama vile upigaji picha, filamu, simulizi na kumbukumbu za safari, maudhui ya mitandao ya kijamii, mashairi, vitabu, pamoja na nyimbo na kasida zenye mada ya Arbaeen.

Wenye nia ya kushiriki wanaweza kuwasilisha kazi zao kupitia tovuti rasmi ya tuzo au kurasa zake za mitandao ya kijamii hadi tarehe 5 Desemba.

Mwaka jana, toleo la kumi la mashindano haya lilipokea kazi 31,824 kutoka nchi 42. Miongoni mwa hizo, kulikuwa na picha 24,464, filamu 359, maudhui 2,500 ya mitandao ya kijamii, simulizi na kumbukumbu 2,100 za safari, mashairi 246, vitabu 87, pamoja na nyimbo au kasida 2,060.

Tuzo ya Kimataifa ya Arbaeen ilianzishwa mwaka 2014 kwa lengo la kuonesha taswira na athari za ziara ya Arbaeen — moja ya mikusanyiko mikubwa zaidi ya kila mwaka duniani.

Arbaeen huadhimishwa na Waislamu wa dhehebu la Shia siku ya arobaini baada ya Ashura, kama kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW). Mamilioni ya wafanyaziyara, hususan kutoka Iraq na Iran, husafiri kwa miguu kuelekea Karbala, Iraq, kutoa heshima, wakiungana na waumini kutoka pembe zote za dunia.

/3494238

captcha