Kwa mujibu wa wizara hiyo, mpango huu wa mafunzo ya kina unalenga kukuza uwezo wa kielimu na maarifa ya kiakili ya maimamu wanaoswalisha kupitia mpangilio wa mafunzo wa miaka mitatu. Takriban maimamu 48,000 watanufaika kila mwaka, Arabi21 imeripoti.
Waziri wa Wakfu Ahmed Toufi, akijibu swali la mbunge, amesema mpango huu unasimamiwa na Baraza Kuu la Maimamu na unajumuisha mafunzo ya kitaaluma kwa maimamu wa jamaa, kuimarisha uwezo wao katika nyanja za mawasiliano na uongozi, pamoja na mafunzo maalumu ya kipekee.
Ameeleza kuwa kiwango cha mahudhurio ya maimamu wa misikiti katika vikao vilivyofanyika mwaka 2025 kilifikia takriban asilimia 94.5 ya walioalikwa, ishara ya mafanikio ya mpango huu na ushirikiano mpana wa washiriki.
Aidha, wizara imetangaza kuanza kwa usajili wa kozi ya 22 ya Taasisi ya Mafunzo ya Maimamu ya Muhammad VI kwa mwaka 2026. Kozi hiyo itahusisha washiriki 150, ambao wanatakiwa kuwa na shahada ya kwanza au sawa na hiyo, wawe chini ya umri wa miaka 45, na wawe wamehifadhi Qur’ani yote.
Muda wa mafunzo katika taasisi hiyo ni miezi 12, ambapo wanafunzi hupokea mshahara wa kila mwezi wa dirham 2,000. Wanaohitimu wanatarajiwa kuajiriwa katika misikiti chini ya mkataba wa ajira.
Kwa mujibu wa Wizara ya Wakfu, mpango wa Mafunzo ya Maimamu unalenga kuwapa viongozi wa dini elimu ya kisheria na ya mawasiliano, kwa mujibu wa misingi ya wastani wa kidini unaoenziwa katika Ufalme wa Morocco.
Wadau wa mpango huu wanasema hatua hii ni mkakati wa kukuza thamani za dini za wastani katika jamii ya Morocco na kuendana na maendeleo ya kisasa katika nyanja za mawasiliano na teknolojia. Kupitia mpango huu, Morocco inalenga kuandaa kizazi kipya cha viongozi wa dini wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kisasa na kulinda utambulisho wa kitaifa na kidini.
/3494236