IQNA

Shule ya Qur'ani ya Novi Pazar: Kituo cha Kufufua Utambulisho wa Kiislamu nchini Serbia

7:39 - August 02, 2025
Habari ID: 3481029
IQNA – Shule ya Qur'ani ya Novi Pazar nchini Serbia ni miongoni mwa vituo muhimu zaidi vya elimu ya Qur'ani katika eneo la Balkan, ikijitahidi kufufua utambulisho wa Kiislamu miongoni mwa Waislamu wa eneo hilo na kuwafundisha Qur'ani Tukufu pamoja na tafsiri yake kwa wenye nia.

Shule hii ya Novi Pazar inaashiria maendeleo ya kielimu na kiroho ya Waislamu wa Ki-Bosnia baada ya miongo kadhaa ya dhuluma ya kidini na juhudi za kufuta utambulisho wao wa Kiislamu.

Tangu ilipoanzishwa mwaka 2010, shule hii imekuwa ni kituo cha Qur'ani ambacho watu wa rika zote wanakusanyika kujifunza Neno la Wahyi, na kizazi baada ya kizazi kuunganishwa na utambulisho wao wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa Sheikh Irfan Malich, Mkurugenzi wa Shule ya Qur'ani ya Novi Pazar, taasisi hii inayosimamiwa na Baraza la Kiislamu la Serbia kwa sasa ina wanafunzi zaidi ya 3,000 wa kiume na wa kike katika matawi zaidi ya 30 kote nchini, ikiwemo mji mkuu Belgrade, pamoja na matawi katika nchi za Ulaya ambako Waislamu wa Bosnia wamehamia.

“Tumeanzisha matawi katika kila mji na kila kijiji ili kuhakikisha hakuna sehemu isiyo na shule ya Qur'ani,” anasema Sheikh Malich, akifafanua kuwa wanafunzi wao wanatoka katika makundi yote ya umri, kuanzia miaka 6 hadi 70, na wote wanaunganishwa na mapenzi yao kwa Qur'ani Tukufu.

Miongo michache iliyopita, kutokana na utawala wa kikomunisti uliodumu hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, ilikuwa ni jambo la kawaida kwa Waislamu wa Serbia kusoma Qur'ani kwa maandiko ya Kilatini. “Wakati huo, hakuna hata mmoja wetu aliyekuwa ameihifadhi Qur'ani,” anasema Malich. Lakini anaongeza kwa fahari, “Sasa tunao maḥafidh (wahifadhi wa Qur'ani), baadhi yao wakiwa wamepewa vyeti vya kuthibitisha utaalamu huo.”

Shule hii hutoa elimu ya Qur'ani kwa ngazi mbalimbali, ikianza na kujifunza herufi za Kiarabu, kisha hukumu za tajwīd na taratibu za usomaji sahihi, hadi kufikia kuhifadhi juzuu za mwisho za Qur'ani, na baadaye wanafunzi kufikia kiwango cha kuhifadhi Qur'ani yote kwa jumla.

Akielezea athari kubwa ya taasisi hii, mwalimu Emilja Alickovic anasema, “Ni neema kutoka kwa Allah kuwa mji wetu una shule ambayo tunasoma Qur'ani kama alivyokuwa akisoma Mtume wetu Muhammad (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam).”

Sima Gecic, mwanafunzi wa Qur'ani katika shule ya Pazar, anasema, “Ninajitahidi kufika hapa kila siku. Hapa ninajifunza Qur'ani, lugha ya Kiarabu na kuelewa dini yangu.”

Ili kuimarisha roho ya ushindani na kuleta motisha, shule hii imeandaa mashindano ya ndani ya Qur'ani mara 11 na pia imeshiriki mashindano ya kimataifa, ikishinda nafasi za juu, ikiwemo nafasi ya kwanza katika moja ya mashindano ya Qur'ani yaliyofanyika Makka.

Katika madarasa ya awali, wanafunzi huanza na herufi, kisha hufundishwa hifadhi na tafsiri, huku wakifundishwa pia maadili ya Kiislamu, anafafanua mwalimu mwingine wa shule hiyo, Jannah Abdullah. “Tunaelezea Surah mbalimbali na kutoa mafunzo ya Kiislamu kutoka humo ili kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kuishi kwa mujibu wa amri za Allah.”

Zaidi ya muongo mmoja tangu kuanzishwa kwake, Shule ya Novi Pazar imekuwa si tu taasisi ya elimu, bali ni nuru ya kiroho inayohifadhi uwepo wa Uislamu nchini Serbia, na kufufua utambulisho wa Kiislamu kwa watu waliokuwa karibu kuupoteza kabisa.

Katika nchi ambayo miongo mitatu iliyopita haikuwa na hata mhifadhi mmoja wa Qur'ani, leo hii – kupitia shule hii – sauti za usomaji Qur'ani zinazidi kusikika, wahifadhi wanahitimu, na vizazi vipya vinaubeba Msahafu wa Allah katika nyoyo zao kupitia kuhifadhi Qur'ani.

3494075

Kishikizo: serbia qurani tukufu
captcha