Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Karbala Alan, Idara ya Qur’ani ya Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS), chini ya usimamizi wa Sekretarieti Kuu, imezindua maonyesho yake ya kila mwaka ya sanaa ya Arbaeen.
Tukio hilo limewekwa karibu na mji wa Imam Hassan al-Mujtaba kando ya njia ya Wafanyaziyara na linaendeshwa na Kituo cha Qalam cha idara hiyo, kinachobobea katika khati ya Kiarabu na sanaa za Kiislamu za jadi.
Wissam al-Delfi, mkuu wa kituo cha habari cha idara hiyo, alisema maandalizi ya maonyesho yalihusisha kukusanya kazi mbalimbali za sanaa za Qur’ani kutoka nchi tofauti, zilizopatikana kupitia maonyesho yaliyopita katika eneo la Bayna al-Haramayn (Kati ya Haram Mbili) mjini Karbala.
“Tumejumuisha pia kazi adimu, kama vile sanamu zilizotengenezwa na wasanii kutoka Indonesia,” alibainisha.
Amesema maonyesho haya yanakusudia kuangazia dhulma alizokumbana nazo Imam Hussein (AS), maneno ya Ahlul-Bayt (AS), na aya za Qur’ani zinazorejelea matukio ya Karbala.
Al-Delfi ameyataja kuwa ni uzoefu wa kiutamaduni na kisanaa kwa pamoja. “Yanaonyesha roho ya Ziyara ya Arbaeen, yakiiunganisha sanaa asilia na ujumbe wa harakati ya Imam Hussein (AS), na kuunda nafasi ya uelewa na mawasiliano katika safari ya Wafanyaziyara,” alisema.
Maonyesho haya hapo awali yalifanyika katika mkoa wa Basra, kwa ushirikiano na tawi la Idara ya Qur’ani huko al-Qurna, ambako yalidumu kwa zaidi ya siku nne kabla ya kuhamishiwa Alhamisi iliyopita katika eneo lake la sasa Karbala.
Yataendelea kuwa wazi hadi baada ya Ziyara ya Arbaeen itakapomalizika.
Al-Delfi aliongeza kuwa maonyesho haya ni sehemu ya programu za kila mwaka za idara hiyo kwa ajili ya njia ya Arbaeen. Lengo lake, amesema, ni kuendeleza utambulisho wa Qur’ani na kuwasilisha ujumbe wa harakati ya Imam Hussein (AS) kwa mtindo wa kisanaa unaochanganya herufi na rangi.
Kila mwaka, mamilioni ya Wafanyaziyara—wengi wao wakiwa kwa miguu—huelekea katika mji wa Karbala nchini Iraq kuadhimisha Arbaeen, siku ya arobaini baada ya shahada ya Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), katika Vita vya Karbala vya mwaka 61 Hijria.
3494192/