IQNA

Rais wa Misri ahimiza ustawishaji wa tovuti ya Idhaa ya Qur’an Tukufu

20:16 - August 15, 2025
Habari ID: 3481085
IQNA – Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri amesisitiza umuhimu wa kuendeleza tovuti ya kimataifa ya Idhaa ya Qur’an Tukufu ya nchi hiyo.

Alhamisi, Abdel Fattah El-Sisi alikutana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Amr Talaat; Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Habari, Ahmed El-Moslemany; pamoja na Meja Jenerali Mohsen Abdel Nabi, mshauri wa rais katika masuala ya habari.

Msemaji rasmi wa Ikulu ya Misri alieleza kuwa katika kikao hicho, Rais El-Sisi alisisitiza haja ya kulinda na kuhifadhi urithi wa redio (Idhaa)na televisheni ya Misri kwa kubadilisha kanda zote za sauti na video zinazomilikiwa na Mamlaka hiyo kuwa mfumo wa kidijitali, na kuwekeza maudhui hayo kupitia jukwaa la kidijitali litakalosimamiwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Habari.

Aidha, msemaji huyo aliongeza kuwa Rais El-Sisi aliagiza kuharakishwa kwa hatua za kuendeleza tovuti ya kimataifa ya Idhaa ya Qur’an Tukufu, ili kuhifadhi urithi wa maqari na mawaidha, pamoja na kulinda vipindi vingi vilivyokuwa vikipeperushwa na Redio ya Qur’an tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964.

Redio ya Qur’an ilianzishwa nchini Misri kwa lengo la kuzuia upotoshaji wa maneno ya Qur’an Tukufu na kutoa qira’ah sahihi kutoka kwa makhari maarufu.

Tangu ilipoasisiwa, Idhaa ya Qur’an imeendelea kupata mapokezi makubwa si tu nchini Misri, bali pia katika nchi nyingi duniani, hususan ulimwengu wa Kiislamu.

3494254

captcha