IQNA

Maadhimisho ya Arbaeen yadhihirisha umoja na msimamo wa Waislamu Dhidi ya Dhulma

23:09 - August 14, 2025
Habari ID: 3481084
IQNA – Katika ziara ya Arbaeen, Waislamu hukusanyika kwa mshikamano ili kufikisha ujumbe wa pamoja wa kusimama imara na kudai haki, amesema afisa wa Kiirani.

Hujjatul-Islam Muhammad-Hassan Akhtari, Mwenyekiti wa Kamati ya Kuunga Mkono Mapinduzi ya Kiislamu ya Watu wa Palestina, iliyo chini ya Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesisitiza umuhimu wa maadhimisho na matembezi ya Arbaeen ya mwaka huu kama alama yenye nguvu ya umoja na msimamo wa kupinga dhulma.

Ameeleza kuwa Arbaeen ni “ishara ya mshikamano na mshikikano miongoni mwa Waislamu na wafuasi wa Ahlul-Bayt (AS), ikionyesha kuwa watu wa dunia wanataka haki na wanapinga uonevu.”

Ameongeza kuwa ziara hii “inatuma ujumbe wa wazi kwa Israel na Marekani kwamba mataifa ya Kiislamu hayatanyenyekea mbele ya mabavu, bali yatasimama na haki na kuyaunga mkono harakati za mapambano za Palestina, Lebanon, Gaza na maeneo mengine.”

Amesema kuwa uwepo huu “unadhihirisha kuwa wao wanafuata madhehebu ya Imam Husayn (AS): madhehebu ya kujitolea shahada na kusimama imara,” na kwamba mataifa ya Kiislamu “yataendelea kukabiliana na dhulma na uhalifu wa mataifa yenye nguvu.”

“Uwepo huu unabeba pia ujumbe kwa wapambanaji wa Palestina, Gaza na Lebanon, kwamba tupo pamoja nanyi na tunasimama bega kwa bega nanyi,” ameongeza.

Amebainisha kuwa Arbaeen “siyo tu maadhimisho ya kidini na kiroho, bali pia ni fursa ya kuimarisha mshikamano, huruma na msimamo dhidi ya maadui wa Uislamu,” huku akitarajia kuwa “harakati hii ya kishujaa itaadhimishwa kwa ukubwa zaidi kila mwaka, ikifikisha ujumbe wake wa amani, haki na msimamo kwa ulimwengu mzima.”

Arbaeen ni siku ya arobaini baada ya Ashura, inayokumbuka kuuawa shahidi kwa Imam Husayn (AS) huko Karbala mwaka 61 Hijiria sawa na 680 BK. Ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa ya kila mwaka duniani kwa amani ambapo mwaka huu, mamilioni ya wafanyaziyara wamekusanyika Karbala, wakisafiri kutoka sehemu mbalimbali za Iraq na nje ya nchi hiyo ili kuonesha mshikamano katika huzuni, imani na msimamo.

Muktadha wa kauli hizi ni ongezeko kubwa la mashambulizi na kampeni ya kuwamaliza kwa njaa watu wa Gaza, ambapo mashambulizi ya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na jeshi katili la Israel yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 61,700, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, tangu Oktoba 2023.

4298909

 

captcha