IQNA

Mwanafunzi wa Kenya aliyeshika nafasi ya kwanza
12:26 - April 15, 2019
News ID: 3471917
TEHRAN (IQNA) – Mashindano ya 36 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya kiwango cha juu sana ikilinganishwa na mashindano mengine yote duniani, amesema Abdulalim Abdulrahim Haji kutoka Kenya ambaye ameshika nafasi ya kwanza ya mashindano ya kuhifadhi Qur'ani maalumu kwa wanafunzi wa shule.

Katika mahojiano maalumu na IQNA, amesema mashindano ya mwaka huu yalikuwa ni magumu kwani washiriki wote walikuwa na uwezo wa juu sana nukta ambayo imeinua kiwango cha mashindano. Aidha Abdulrahim Haji amebaini kuwa nukta za kipekee za mashindano ya mwaka huu ni nidhamu ya hali ya juu pamoja na jopo la majaji wataalamu kutoka nchi mbali mbali ambao wamefanya kazi yao kitaalamu. Ameongeza kuwa  hata wale ambao hawakuweza kushinda katika duru hii ya mashindano wamepta uzoefu mzuri wa kushiirki katika mashindano ya siku za usoni.

Kuhusiana na nafasi Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuleta umoja na mshikamano wa Waislamu duniani, amebaini kuwa mashindano yote yana nafasi nzuri ya kuimarisha umoja baina ya Waislamu. Ameongeza kuwa: "Wakati washiriki kutoka nchi mbali mbali wanapoalikwa a kushiriki katika mashindano kama haya, jambo hilo huweza kuzidisha umoja. Katika mashindano haya, kuna washiriki kutoka nchi mbali mbali na tumeona namna Waislamu wa mabara ya Ulaya, Asia na Afrika walivyojumuika hapa jambo ambalo linaleta umoja baina yao."

Abdulrahim Haji ametoa wito kwa vijana Waislamu nchini Kenya na ulimwengu mzima kwa ujumla kujitahidi kuhifadhi Qur'ani na waliohifadhi wadumishe amali hiyo njema na wajitahidi kutekeleza mafundisho ya Qur'ani kivitendo. Ameongeza kuwa kufungamana na Qur'ani ndio msingi wa kudumisha umma wa Kiislamu na chanzo cha saada ya Mwislamu duniani na akhera na hivyo kumfanya mja atukuke mbele ya Mwenyezi Mungu.

Washiriki 184 wa mashindano ya Qur'ani kutoka nchi 84 walifanikiwa kufika katika nusu fainali ya mashindano ya mwaka huu.

Nusu fainali ya mashindano hayo ilifanyika Jumanne Aprili 9 na Jumatano Aprili 10 asubuhi kabla ya ufunguzi rasmi wa fainali alasiri ya Jumatano ambapo mashindano yamemalizika Aprili 14.

Washindi wametunukiwa zawadi katika sherehe ambazo zimefanyika katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA hapa Tehran ambao pia ulikuwa mwenyeji wa mashindano ya wanaume huku ya wanawake yakiwa yamefanyika katika ukumbi mwingine maalumu.

Shirika la Wakfu la Iran huandaa mashindano ya kimatiafa ya kusoma na kuhifadhi Qur'ani ya Iran kila mwaka ambapo huwa na washiriki kutoka kila kona ya dunia.

Hapo chini ni video ya Qiraa ya Abdulalim Abdulrahim Haji  katika mashindano 

Name:
Email:
* Comment: