IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
9:17 - April 16, 2019
News ID: 3471918
TEHRAN (IQNA) -Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, baadhi ya watawala wa nchi za Kiislamu hawatekelezi maamrisho ya Qur'ani na ni vibaraka wa Marekani na Wazayuni.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo Jumatatu  hapa mjini alipokutana na washiriki wa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani  na kusisitiza kuwa, kuifanyia kazi Qur'ani Tukufu kunaandaa uwanja wa kupatikana izza (heshima), ustawi, maendeleo, nguvu, mshikamano, mtindo mzuri wa maisha katika dunia na kudhaminiwa saada na ufanisi wa Akhera.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu  amebainisha kwamba, baadhi ya viongozi wa nchi za Kiislamu wamekuwa chanzo na chimbuko la hitilafu, mifarakano na vita kama vya Syria, Yemen na kuuawa Waislamu.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, matatizo na masaibu mengi ya Umma wa Kiislamu na jamii ya wanadamu yanatokana na kutoyafanyia kazi maarifa ya Qur'ani Tukufu.

Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, hii leo kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hali ya wananchi hasa vijana kuyapokea na kushikamana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku; na kwamba, hii hali ya kushikamana na Qur'ani Tukufu ndio itakayokuwa chimbuko la saada, nguvu na heshima ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei, ameashiria uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kwamba, licha ya kuwa uadui huo umeongezeka kuliko huko nyuma, lakini inaonekana kuwa, hatua na njama hizi zinavuta pumzi zake za mwisho.

 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei pia amesema: "Kadiri adui anavyoshadidisha uhasama dhidi ya taifa la Iran na kadiri anavyokuwa mgumu zaidi na kadiri anavyozidi kupandwa na hasira kutokana na taifa la Iran kufungamana na Qur'ani, mkabala wa hilo, taifa hili litazidi kuwa na uwezo na nguvu zaidi na litashikamana zaidi na Qur'ani Tukufu.

Washiriki 184 wa mashindano ya Qur'ani kutoka nchi 84 walifanikiwa kufika katika nusu fainali ya mashindano ya mwaka huu.
Nusu fainali ya mashindano hayo ilifanyika Jumanne Aprili 9 na Jumatano Aprili 10 asubuhi kabla ya ufunguzi rasmi wa fainali alasiri ya Jumatano ambapo mashindano yamemalizika Aprili 14.

Washindi wametunukiwa zawadi katika sherehe ambazo zimefanyika katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA hapa Tehran ambao pia ulikuwa mwenyeji wa mashindano ya wanaume huku ya wanawake yakiwa yamefanyika katika ukumbi mwingine maalumu.

Shirika la Wakfu la Iran huandaa mashindano ya kimataifa ya kusoma na kuhifadhi Qur'ani ya Iran kila mwaka ambapo huwa na washiriki kutoka kila kona ya dunia.

3803809

 

Name:
Email:
* Comment: