IQNA

12:15 - April 18, 2019
News ID: 3471920
TEHRAN (IQNA)-Qarii wa Qur'ani Tukufu kutoka Kenya ambaye ameshiriki katika Mashindano 36 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran amesema mashindano hayo yanaimarisha umoja baina ya Waislamu.

Katika mahojiano maalumu na IQNA, Qarii Salim Mohammad Salim ambaye alishiriki katika kitengo cha Qiraa maalumu kwa ajili ya wanafunzi katika mashindano hayo ameongeza kuwa: "Waislamu wanahitaji umoja na Qur'ani inatuunganisha sote. Waislamu wote, wawe ni Shia au Sunni wanapaswa kuungana kwani iwapo watafrikiana basi Marekani itapata fursa ya kujipenyeza na kutumaliza."

Huku akisisitiza umuhimu wa Waislamu kuungana, Qarii Salim Mohammad Salim ambaye ni mwenyeji wa Mombasa ameongeza kuwa, kwa baraka ya Qur'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu atauhifadhi Uislamu.

Akiashiria kiwango cha mashindano ya kimataifa ya Qur'ani mwaka huu nchini Iran Qarii Mohammad Salim ambaye amewahi kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani nchini Misri na Uturuki amesema: "Kiwango cha mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Iran ni cha juu sana kuliko mashindano ambayo nimewahi kushiriki."

Kuhusiana na harakati za Qur'ani nchini Kenya Qarii Mohammad Salim amesema, "kiwango cha kuhifadhi Qur'ani nchini Kenya ni cha juu sana lakini kuna haja ya kuimarisha qiraa." 

Washiriki 184 wa mashindano ya Qur'ani kutoka nchi 84 walifanikiwa kufika katika nusu fainali ya mashindano ya mwaka huu.

Nusu fainali ya mashindano hayo ilifanyika Jumanne Aprili 9 na Jumatano Aprili 10 asubuhi kabla ya ufunguzi rasmi wa fainali alasiri ya Jumatano ambapo mashindano yamemalizika Aprili 14.

Washindi walitunukiwa zawadi katika sherehe ambazo zimefanyika katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA hapa Tehran ambao pia ulikuwa mwenyeji wa mashindano ya wanaume huku ya wanawake yakiwa yamefanyika katika ukumbi mwingine maalumu.

Abdulalim Abdulrahim Haji kutoka Kenya alishika nafasi ya kwanza ya mashindano ya kuhifadhi Qur'ani maalumu kwa wanafunzi wa shule.

Shirika la Wakfu la Iran huandaa mashindano ya kimatiafa ya kusoma na kuhifadhi Qur'ani ya Iran kila mwaka ambapo huwa na washiriki kutoka kila kona ya dunia.

Name:
Email:
* Comment: