IQNA

11:22 - April 30, 2019
News ID: 3471935
TEHRAN (IQNA)- Duru ya 12 ya mashindano ya kimataifa ya kusoma Qur'ani (qiraa) ambayo hufanyika mubashara au moja kwa moja kupitia Televisheni ya Al Kauthar ya Iran yanatazamiwa kuwa na washiriki 250 mwaka huu.

Hayo yamedokezwa na Sayyed Abbas Razavi, afisa mwandamizi wa Televisheni ya Al Kauthar wakati akizungumza na waandishi habari mjini Tehran.
Mashindano hayo yaliyopewa anuani ya إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ مَفَازًا , "Hakika wachamngu wanastahiki kufuzu" hufanyika kwa njia ya simu na kuanza katika usiku kwa kwanza wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kila mwaka.
Sayyed Razavi amesema washiriki 96 wanatazamiwa kuingia nusu fainali na hatimaye watano miongoni mwao wataingia fainali. Watakaofanikiwa kufika fainali wataalikwa katika makao makuu ya Televisheni ya Al Kauthar mjini Tehran kushiriki katika fainali ya mashindano hayo ya qiraa ya Qur'ani Tukufu.
Aidha ameongeza kuwa nchi kama vile Misri, Iran, Iraq, Syria na Lebanon zina washiriki wengi zaidi katika duru ya mashindano ya mwaka huu. Fainali zinatazamiwa kufanyika katika usiku wa kuamkia Idul Fitr. Kwa mujibu wa Sayyed Razavi, jopo la majaji wanaojumuisha wataalamu wa Qur'ani Tukufu kutoka Iran na nchi kadhaa wanatazamiwa kusimamia mashindano hayo ya Qur'ani.
Mashindano hayo, ambayo ni makubwa zaidi ya aina yake duniani, yatakuwa yanarushwa hewani kuanzia saa tano unusu usiku(23:30) kwa wakati wa Tehran au saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki kupitia Televisheni ya Kimataifa ya Al Kauthar na fainali zitafanyika katika siku ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Televisheni ya Al Kauthar ni katika televisheni zinazosimamiwa na Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa maelezo zaidi kuhusu mashindano hayo na namna ya kujisajili, bonyeza hapa.

3807374

Name:
Email:
* Comment: