IQNA

Televisheni ya Qur'ani ya Misri yatangaza vipindi maalum kwa ajili ya Ramadhani

20:58 - February 18, 2025
Habari ID: 3480234
IQNA – Televisheni ya Qur'ani ya Misri itarusha vipindi mbalimbali vya Qur'ani ili kuongeza hali ya kiroho katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Misrawi, vipindi hivyo vitajumuisha usomaji bora wa Qur'ani kutoka kwa wasomaji maarufu ambao hawajawahi kurushwa hewani hapo awali.

Zaidi ya hayo, Qur'ani itasomwa kwa sauti nadra za Sheikh Muhammad Rif’at kabla ya adhana za asubuhi na jioni.

Mtandao huu wa televisheni utakuwa na kipindi cha kipekee cha takriban saa moja cha usomaji wa Qur'ani kutoka kwa Sheikh Ragheb Mustafa Ghalwash, Sheikh Shaaban Mahmoud al-Sayyad, na Sheikh Muhammad Mahmoud al-Tablawi.

Kila usiku saa nne , juzuu moja kamili ya Qur'ani itasomwa na wasomaji mashuhuri wa Misri, wakiwemo Sheikh Abdul Basit Abdul Samad, Sheikh Mahmoud Ali al-Banna, Sheikh Muhammad Siddiq al-Minshawi, Sheikh Mustafa Ismail, Sheikh Mahmoud Khalil al-Hussary, Sheikh Muhammad al-Hussary, na wengineo.

Usomaji kamili wa Qur'ani nzima utarushwa kila baada ya siku mbili, ukiambatana na ufafanuzi wa msamiati wa aya wakati wa usomaji.

Aidha, qiraa 391 nadra kutoka kwa wasomaji 13 mashuhuri wa miaka ya 1990 zitarushwa hewani, wakiwemo Sheikh Muhammad al-Saifi, Sheikh Abulainain Shuaisha, Sheikh Abdul Rahman Al-Duri, Kamel Youssef al-Bahtimi, Sheikh Abdul Fattah al-Shaasha'i, Sheikh Ahmed Suleiman al-Saadani, Sheikh Mansour al-Shami al-Damanhuri, Sheikh Abdul Basit Abdul Samad, Sheikh Mustafa Ismail, Sheikh Mahmoud Ali Al-Banna, Sheikh Muhammad Siddiq al-Minshawi, Sheikh Abdul Azim Zahir, na Sheikh Mahmoud Khalil al-Hussary.

Pia, usomaji wa Qur'ani kutoka kwa wasomaji chipukizi waliothibitishwa na kamati ya mitihani ya pamoja ya Umoja wa Redio na Televisheni ya Misri utapeperushwa hewani.

Ramadhani ni mwezi wa tisa na mtukufu zaidi katika kalenda ya Kiislamu, ambapo Waislamu huadhimisha ufunuo wa Qur'ani kwa Mtume Muhammad (SAW).

Katika mwezi wa Ramadhani, Waislamu hufunga kuanzia alfajiri hadi machweo, wakijizuia kula, kunywa, kuvuta sigara na kushiriki mahusiano ya ndoa.

Wakati huo huo, wanajitolea zaidi kwa ibada, kutoa sadaka na kutenda mema kwa lengo la kuimarisha imani na kujisafisha kiroho.

Mojawapo ya desturi za Ramadhani ni kusoma na kujifunza Qur'ani, ambapo baadhi ya Waislamu hujitahidi kuikamilisha Qur'ani nzima ndani ya mwezi huu mtukufu.

Mwaka huu, siku ya kwanza ya Ramadhani inatarajiwa kuwa tarehe 1 Machi.

3491897

captcha