IQNA

14:57 - June 03, 2019
News ID: 3471983
TEHRAN (IQNA)- Hali si shwari nchini Sudan. Taarifa kutoka Khartoum, mji mkuu wa nchi hiyo zinaarifu kuwa, kwa akali watu watano wameuawa baada ya maafisa usalama nchini humo kushambulia kwa risasi hai maandamano ya wananchi wanaolalamikia hatua ya jeshi la nchi hiyo kung'ang'ania madaraka.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, makabaliano hayo kati ya waandamanaji wanaotaka kuundwa serikali ya kiraia na maafisa usalama yamefanyika mapema leo Jumatatu nje ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Khartoum.

Waandamanaji hao wenye ghadhabu wamefunga barabara zote muhimu mjini Khartoum, huku wakiapa kuendelea kukita kambi nje ya makao makuu hayo ya jeshi licha ya kushambuliwa kwa risasi hai na mabomu ya kutoa machozi.

Jana Jumapili pia, polisi na jeshi la nchi  hiyo waliwashambulia kwa risasi wananchi walioendeleza maandamano na kukusanyika mbele ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo katika mji mkuu Khartoum na kumuua kijana mmoja wa miaka 20 na kujeruhi wengine 10.

Makundi ya mawili yanayoongoza maandamano hao ya raia nchini Sudan, yaani Jumuiya ya Wanataaluma wa Sudan na "Muungano wa Makundi ya Ukombozi na Mabadiliko" ambao ndio muungano mkubwa zaidi wa wapinzani huko Sudan yametoa taarifa tofauti na kulaani hatua ya jeshi la Sudan ya kuwashambulia kwa risasi waandamanaji, kufanya mauaji, kuwagonga kwa magari na kuwapiga marungu raia wanaoandamana kwa amani yakisisitiza kuwa, lengo la wanajeshi hao wa Sudan lilikuwa ni kuua.

Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan limeonya kuhusu kuundwa serikali ya kiraia nchini humo hivi sasa na kudai kuwa, jambo hilo litazidisha machafuko nchini humo.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia na Imarati ni waungaji mkono wakubwa wa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan ambalo linaendelea kung'ang'ania madaraka. Baraza hilo lilitwaa uongozi wa nchi tarehe 11 Aprili baada ya kufanya mapinduzi ya kijeshi yaliyomng'oa madarakani Omar al-Bashir. Makundi ya wapinzani nchini humo yametangaza kuendeleza maamdamano yao. Raia wa Sudan pia wanataka kuhitimishwa uwepo wa askari wa nchi hiyo katika muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen.

3816849

Name:
Email:
* Comment: