IQNA

10:50 - June 20, 2019
News ID: 3472008
TEHRAN (IQNA) – Mchunguzi maalumu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa ushahidi unaonyesha mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia na maafisa kadhaa wa ngazi ya juu wa ufalme huo walihusika na mauaji ya mwandishi habariJamal Khashoggi.

Ripoti ya mtaalamu huyo wa UN Agnes Callamard inasema kuwa ushahidi huo unahitaji kufanyiwa uchunguzi na jopo huru la kimataifa lisilipoendelea upande wowote.

Akizungumza Jumatano mjini Geneva, Callamard amesema kuwa upo ushahidi wa kutosha unaoeleza namna maafisa wa ngazi ya juu wa Saudia akiwemo Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo walivyohusika katika mauaji ya Jamal Khashoggi mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Aal Saud.

Ripoti hiyo yanye kurasa 101 juu ya mauaji ya Khashoggi kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki, inatoa mwito kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa au Katibu Mkuu Antonio Guterres, kufungua uchunguzi zaidi wa uhalifu.

Callamard amesema uchunguzi wake umebaini kwamba kuna ushahidi wa kuaminika, unaoruhusu uchunguzi zaidi wa maafisa wa ngazi ya juu wa Saudi Arabia, akiwemo mrithi wa ufalme.

"Nilichonacho ni ushahidi unaoonyesha kuhusika kwa maafisa wa ngazi ya juu na hivyo kuhitaji uchunguzi zaidi, hasa dhidi ya mrithi wa ufalme kwa sababu mbalimbali, na kubwa kabisaa kwa kuwa watu waliohusika na mauji hayo waliripoti kwake moja kwa moja."

Khashoggi,aliyekuwa na umri wa miaka 58 , na aliyekuwa akiandikia gazeti la the Washington Post na mkosoaji mkubwa wa mwanamfalme Mohammed mara ya mwisho alionekana akiingia katika ubalozi wa Saudia tarehe 2 Oktoba 2018 ili kuchukua nakala alizohitaji ili kumuoa mchumba wake Hatice Cengiz. Callamard alisema kuwa Khashoggi aliuawa kikatili ndani ya ubalozi huo.

Akizungumza baada ya kutangazwa ripoti hiyo, Rais Recep Tayyip Erdogan aliwalaani vikali waliomuua Khashoggi na kusema watawajibishwa. Akizungumza mjini Istanbul, amesema ripoti hiyo imethibitisha kuwa utawala wa Saudi Arabia ulihusika katika mauaji hayo.

3468790

 

Name:
Email:
* Comment: