IQNA

21:46 - September 10, 2019
News ID: 3472124
TEHRAN (IQNA) - Jeshi la Nigeria limeua Waislamu wasiopungua 12 waliokuwa katika maombolezo ya Siku ya Ashura (tarehe 10 Muharram) wakikumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS.

Taarifa iliyotolewa na Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) imesema kuwa, askari wa serikali ya Nigeria wamewafyatulia risasi Waislamu walioshiriki katika shughuli ya maombolezo ya Ashura na kuua Waislamu wasiopungua 12 na kujeruhi makumi ya wengine.
Ibrahim Musa, msemaji wa IMN, ambayo aghalabu ya wanachama wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia amesema utawala wa Nigeria umewakandamiza wanachama wa harakati hiyo kitaifa. Ameongeza kuwa mauaji ya leo yamejiri baada ya jeshi kuwalenga Waislamu waliokuwa wakishiriki katika hafla za Siku ya Ashura katika majimbo ya Kaduna, Bauchi, Sokoto na Katsina. Taarifa hiyo imesema maombolezo ya Ashura yamefanyika kwa amani katika majimbo mengine ya Nigeria kama vile huko Abuja, Jos, Kebbi, Minna, Lafia, Yola, Gusau, Zaria, Kano, Jalingo, Damaturu, Hadejia na Potiskum.Maafisa wa usalama wa Nigeria walikuwa wametoa taarifa na kusema watakaoshiriki katika maombolezo ya Ashura ni 'magaidi' kutokana na kuwa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imepigwa marufuku.
Siku ya Ashura ni siku ya 10 ya Muharram ambao ni mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislamu ya Hijria Qamaria. Waislamu wa madhehebu ya Shia na wengine kote duniani hujumuika katika siku 10 za kwanza za Muharram kuomboleza kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu. Imam Hussein AS aliuawa shahidi katika siku ya Ashura.
Hii si mara ya kwanza kwa askari wa Nigeria kushambulia umati wa Waislamu waliokuwa wakishiriki katika shughuli ya maombolezo na kukumbuka mauaji ya Imam Hussein (as). Mwaka jana pia jeshi la Nigeria lilishambulia mjumuiko mkubwa wa Waislamu walioshiriki maombolezo ya siku ya Ashura katika mji wa Zaria huko kaskazini mwa Nigeria na kuua shahidi watu kadhaa.
Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika na jeshi la nchi hiyo hata baada ya mahakama kuamuru waachiliwe huru.
Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo.
Wiki iliyopita, afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesghulikia masuala ya hukumu zisizofuata sheria na pia mauaji ya kiholela, Agnes Callamard, aliilaani serikali ya Nigeria kwa kutekeleza mauaji na kutumia nguvu ziada dhidi ya Harakati ya Kiislamu nchini humo.
Callamard pia alikosoa alichosema ni kunyimwa maisha kwa mabavu na utumiaji wa nguvu kupita kiasi dhidi ya mikusanyiko ya wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Alisema hatua ya kupigwa marufuku harakati hiyo ya Kiislamu inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky ilitegemea dhana tu na kwamba hajapewa ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa kundi hilo lina silaha au ni hatari kwa Nigeria.

3841339

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: