IQNA

Katika mahojiano na IQNA
14:35 - December 15, 2019
News ID: 3472279
TEHRAN (IQNA) – Suhaila Zakzaky, bintiye Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria (IMN) ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuishinikiza serikali ya Nigeria kumuachilia huru mwanazuoni huyo wa Kiislamu.

Katika mahojiano na IQNA, ameeleza masaibu anayokumbana nayo baba yake aliyeko gerezani na kuashiria sababu zilizopelekea asiachiliwe huru mpaka sasa.

Suhaila Zakzaky amesema kuwa, serikali ya Nigeria inakiuka sheria za ndani na za kimataifa kwani licha ya mahakama kutoa amri ya kuachiliwa huru baba yake, lakini vyombo vya usalama vimeendelea kumshikilia mwanazuoni huyo huku vikishadidisha ukandamizaji dhidi ya wafuasi wake.

Kuhusiana na ukandamizaji unaofanywa na serikali ya Nigeria dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, Suhaila Zakzaky amesema kuwa, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imekuwa ikikabiliwa na mashinikizo tangu ilipoasisiwa na hilo linatokana na misimamo Sheikh Zakzaky za kutaka mageuzi na kupigania kwake uadilifu.

Aidha amesema anataraji kuwa, mataifa ya dunia na asasi za haki za binadamu zitaishinikiza serikali ya Rais Muhamadu Buhari na kuifanya iheshimu sheria.

Siku chache zilizopita Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna nchini Nigeria ilikubali ombi la gavana wa jimbo hilo la kupelekwa kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe katika jela kuu ya jimbo hilo.

Hivi karibuni Nasser Umar Safir daktari wa Sheikh Ibrahim Zakzaky alisema kuwa msomi huyo ameathiriwa na sumu na anapaswa kupewa matibabu haraka iwezekanavyo na kwamba, kuendelea kuwepo hai Sheikh Zakzaky licha ya hali yake mbaya ya kiafya ni jambo linalofanana na muujiza.

Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kushambulia Hussainiyah iliyoko katika mji wa Zaria. Katika shambulio hilo, Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria wasiopungua 1,000, wakiwemo wana watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi.

Baada ya jitihada kubwa, maandamano ya kila pembe na mashinikizo mengi ya ndani na kimataifa, mnamo mwezi Agosti, mahakama ya Nigeria iliruhusu Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wapelekwe India kutibiwa, lakini kutokana na matatizo na vizuizi vilivyowekwa na maafisa wa usalama walioandamana naye, kiongozi huyo wa kidini pamoja na mkewe waliamua kurudi Nigeria baada ya kukaa India kwa muda wa siku mbili tu pasi na kupatiwa matibabu.

Kabla ya hapo, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ilikuwa imefichua kwamba, serikali ya nchi hiyo imekula njama ya kumuua Sheikh Zakzaky kwa kutumia mbinu tofauti ikiwemo ya kumpa sumu.

3862956

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: