IQNA

13:27 - September 18, 2019
News ID: 3472136
TEHRAN (IQNA) Waislamu wasiopungua laki sita wa jamii ya Rohingya waliosalia nchini Myanmar wangali wanakabiliwa na hatari kubwa ya kuuliwa kwa kimbari.

Katika ripoti yao maalumu waliyotoa hapo wiki hii, wachunguzi wa tume ya Umoja wa Mataifa ya kutafuta ukweli wamesema, jeshi la Myanmar lingali linaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na kwamba Waislamu hao wanaendelea kukabiliwa na hatari kubwa ya kuangamizwa kizazi chao.

Tume ya Umoja wa Mataifa ya kutafuta ukweli ambayo iliundwa mwezi Machi mwaka 2017 na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imebainisha katika ripoti yake hiyo kwamba, kwa hali ilivyo hivi sasa, ni jambo 'lisilowezekana' kwa Waislamu milioni moja Warohingya, ambao walilazimika kuihama Myanmar kutokana na ukandamizaji wa jeshi kurejea tena nchini humo.

Kabla ya hapo wachunguzi hao wa Umoja wa Mataifa walitangaza kuwa, operesheni ya hujuma na mashambulio yaliyofanywa mwaka 2017 na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu Warohingya yalikuwa ni "mauaji ya kimbari" na wakataka majenerali waandamizi wa jeshi hilo hususan mkuu wa jeshi la nchi hiyo Min Aung Hlaing wapandishwe kizimbani na kufunguliwa mashtaka ya kuua, kubaka wanawake kimagenge na kuchoma moto makazi ya raia.

Ripoti ya hiyo ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa imebainisha pia kuwa, serikali ya Myanmar imekanusha jinai ilizofanya; na kwa hatua yake ya kujaribu kufuta ushahidi inataka kukwamisha kufanyika uchunguzi athirifu kuhusu hali ya sasa ya Waislamu Warohingya katika jimbo la Rakhine.

Serikali ya Myanmar haiwatambui Waislamu Warohingya kuwa ni raia wa nchi hiyo.

Tume ya kutafuta ukweli ya Umoja wa Mataifa imesisitiza tena udharura wa Baraza la Usalama la umoja huo kuifikisha Myanmar kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) au kuiundia mahakama maalumu ya kufuatilia jinai zake kama ilivyofanyika kwa mauaji ya kimbari ya Yugoslavia ya zamani na Rwanda.

Agosti 25 mwaka 2017 Waislamu wapatao 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya vikosi vya jeshi la Myanmar kuanzisha wimbi kubwa la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.

Maandamano ya Jumapili yalifanyika siku kadhaa baada ya jaribio la pili lililofeli la kuwarejesha wakimbizi hao, ambalo halikushuhudia hata Mrohingya mmoja aliyevuka mpaka kwa hiari na kurejea Myanmar.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, imesema inatafakari kuhusu kuanzisha uchunguzi kuhusu ukatili wanaotendewa Waislamu wa jamii ya Rohingya.

3469419

Name:
Email:
* Comment: