IQNA

21:21 - November 06, 2019
News ID: 3472202
TEHRAN (IQNA) - Kinara wa magaidi wakufurishaji wanaofungamana na mtandao wa Al Qaeda ameuawa nchini Mali katika oparesheni ya kijeshi.

Akizungumza Jumanne akiwa nchini Mali, Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Florence Parly ametangaza kuwa  Abou Abderahman al Maghrebi aliyekuwa na lakabu ya Ali Maychou na ambaye alikuwa  kinara wa kundi la wakufurishaji linalojiita Jama'a Nusrat ul-Islam wa al-Muslimin' (JNIM), ambalo linafungamana na Al Qaeda, aliuawa Oktoba 8 katika oparesheni ya pamoja na wanajeshi wa Mali na Ufaransa.

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa alikuwa pia mjini Ouagadougou nchini Burkina Faso kuhudhuria kikao cha Kundi la 5 la Sahel kwa lengo la kuratibu oparesheni za kijeshi zinazojulikana kama Bourgou 4. Oparesheni hizo zilianza Jumanne nchini Burkina Faso kufuatia hujuma kadhaa za kigaidi karibuni katika nchi za ukanda wa Sahel magharibi mwa Afrika. Oparehseni hizo zinajumuisha majeshi ya Burkina Faso, Mali, Niger na pia askari kutoka Ufaransa.

Siku chache zilizopita maafisa wa serikali ya Burkina Faso walitangaza kuwa, watu 16 waliuawa katika shambulizi la kigaidi kaskazini mwa nchi hiyo.

Tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa, magenge ya kigaidi yameongeza mashambulizi yao katika maeneo mbalimbali hasa ya kaskazini na mashariki mwa Burkina Faso. Hadi hivi sasa watu wasiopungua 570 wameshauawa kwenye mashambulio hayo.

Kuanzia mwaka 2013, wanajeshi wa Ufaransa, chini ya kisingizio cha kupambana na ugaidi, waliingia katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi lakini uwepo wao haujapunguza hujuma za kigaidi bali kumeshuhudiwa kuuawa idadi kubwa ya raia katika mashambulizi ya kigaidi katika eneo hilo.

3855182

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: