IQNA

Saudi Arabia yatangaza marufuku ya Umrah kutokana na kirusi cha Corona

13:19 - March 05, 2020
Habari ID: 3472533
TEHRAN (IQNA) - Saudi Arabia imewapiga marufuku raia wake na wakazi wa nchi hiyo kutekeleza ibada ya Umrah katika mji Mtakatifu wa Makka au kuzuru Msikiti wa Mtume SAW katika mji wa Madina kwa hofu ya kuenea kirusi cha Corona ambacho kinaenea kwa kasi duniani.

Uamuzi huo unakuja baada ya ule wa siku chache zilizopita wa kuwapiga marufuku raia wa kigeni kutekeleza Ibada ya Umrah na Ziara katika Msiktii wa Mtume SAW.

Katika taarifa rasmi siku ya Jumatano, Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesema imeama: "Tumeamua kusitisha kwa muda Umrah kwa raia na wakaazi wa Saudia. Aidha Ziara katika Msikitiw a Mtume mjini Madina ni marufuku."

Taarifa hiyo imesema lengo la uamuzi huo ni kuzuia kuenea kirusi cha Corona katika misikiti miwili mitakatifu ya Makka na Madina ambayo kwa kawaida hushuhudia msongamano mkubwa wa waumini. 

Kumekuwa na wasiwasi kuwa Saudi Arabia, ambayo hupokea karibu waumini milioni 7 kila mwaka kwa ajili ya Ibada ya Umrah, haijakuwa na uwazi kuhusu namna kirusi cha Corona kilivyoiathiri nchi hiyo.

Saudi Arabia iliripoti kesi yake ya pili ya Corona Jumatano na kudai kuwa muathirika alikuwa ni raia wa Saudia aliyerejea kutoka Iran akipitia Bahrain.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, hadi sasa zaidi ya watu elfu 95 wameathirika na kirusi cha Corona kote duniani ambapo kati yao watu elfu 45 wamepona huku wengine zaidi ya 3,286  wakifariki dunia. Korea Kusini na Italia ni kati ya nchi zilizoathriwia zaidi na Kirusi cha Corona baada ya China ambapo hadi sasa watu 107 wamepoteza maisha Italia kutokana na ugonjwa huo huku walioambukizwa Korea Kusini wakifika 5,766. Marekani pia inaonekana kuathiriwa vibaya baada ya jimbo la California kutangaza hali ya hatari huku hadi sasa watu 11 wakiripotiwa kufariki nchini humo kutokana na kirusi cha Corona. 

Iran ambayo pia ni miongoni mwa nchi zilizoasthiriwa na Corona iko mstari wa mbele kwa kufanya kazi usiku na mchana katika kupambana na kirusi hicho kinachoenea kwa kasi. Aidha wataalamu nchini Iran wako mbioni kuunda chanjo ya kirusi cha Corona aina ya COVID-19 na inatarajiwa kuwa katika siku zijazo watatangaza mafanikio katika uga huo.

3883310/

captcha