IQNA

Hija na Umrah

Sasa ni rukhsa kufunga ndoa rasmi katika maeneo matakatifu zaidi ya Uislamu

17:29 - January 28, 2024
Habari ID: 3478266
IQNA - Msikiti Mkuu wa Makkah yaani Masjid al-Haram na Msikiti wa Mtume SAW, yaani Al Masjid An Nabawi huko Madina sasa ina idhini ya kuwa mwenyeji wa kufungisha ndoa au Nikah, kulingana na ripoti.

Mamlaka ya Saudia imeruhusu  kufungisha ndoa katika maeneo mawili matakatifu zaidi ya Uislamu huko Makka na Madina kama sehemu ya mipango iliyozinduliwa ili kuimarisha suhula kwa Waislamu kutoka kote dunaini wanaofika katika maeneo hayo matakatifu kwa ajili ya ibada za Hija na Umrah..

Gazeti la Al Watan la Saudia limeandika kwamba mpango huo ulizinduliwa na Wizara ya Hajj na Umrah na unaruhusu kufungisha ndoa kwa nidhamu maalumu jambo ambalo litabakisha kumbukumbu nzuri kwa Waislamu watakaofunga ndoa wakati  wakiwa katika  Masjid al-Haram na Al Masjid An Nabawi.

Wataalamu wameuita mpango huo kuwa "fursa" kwa makampuni ya huduma za Hija na Umrah kuja na mawazo ya kibunifu ya kuandaa matukio kama haya kwa kuzingatia heshima ya maeneo hayo mawili matakatifu.

Bw. Musaed Al Jabri ambaye ni Mazoun, au afisa wa ndoa Saudia, alisema kufungisha ndoa katika Masjid al-Haram inaruhusiwa katika Uislamu, akisema kwamba Mtume Muhammad (SAW) alisimamia shughuli ya Nikah ya sahaba mmoja  katika msikiti huo.

Al Jabri alibainisha kuwa kufungisha ndoa  katika Msikiti wa Mtume tayari ni jambo la kawaida miongoni mwa wenyeji wa Madina.

"Hii ni kutokana na sababu kadhaa," alisema. “Baadhi yao wana desturi ya kuwaalika watu wengi wa ukoo wa wanaooana. Mara nyingi, nyumba ya familia ya mke-mke haiwezi kubeba walioalikwa wote. Kwa hivyo, Nikah hufanyika katika Msikiti wa Mtume au Msikiti wa Quba (msikiti wa kwanza kujengwa katika Uislamu)," aliongeza.

Baadhi ya watu, alisema, wanaamini kwamba kufunga ndoa katika misikiti hiyo mitakatifu huleta "baraka na bahati nzuri".

Kuhusu sheria ambazo wahudhuriaji wa hafla za ndoa  wanapaswa kuzingatia, alisema ni pamoja na kuzuia usumbufu wa waumini wengine kwa sauti kubwa na shamra shamra. "Pia ni muhimu kuzingatia utakatifu wa mahali hapo na kuepuka kuleta kahawa nyingi, peremende, au chakula," Al Jabri aliongeza.

Mamilioni ya Waislamu kutoka ndani na nje ya Saudi Arabia kila mwaka huenda kwenye Msikiti Mkuu wa Makka kutekeleza Hija na Umra na kutembelea Msikiti wa Mtume na alama nyingine za Kiislamu huko Madina.

3486980

 

Kishikizo: umrah saudia nikah
captcha