IQNA

15:12 - March 12, 2020
News ID: 3472558
TEHRAN (IQNA) - Rais Muhammad Ashraf Ghani wa Afganistan ametoa amri ya kuachiliwa huru kutoka gerezani wafungwa ambao ni wanachama wa kundi la wanamgambo wa Taliban

Sidiqi Sidiqi, msemaji wa Rais Ashraf Ghani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter: Ashraf Ghani ametia saini agizo lenye vipengee 14 la kuachiliwa huru wafungwa wa Taliban hatua ambayo imefanyika kwa lengo la kuanza mazungumzo ya amani nchini humo. Kwa mujibu wa agizo hilo, kuanzia wiki ijayo wafungwa wa kundi la Taliban wataanza kuachiliwa huru. Iliamuliwa kuwa, wafungwa wapatao 5,000 wa Taliban wataachiliwa kutoka katika magereza ya serikali ya Afghanistan. Hata hivyo katika hatua ya awali, ni wafungwa 1500 tu wa kundi hilo wataachiliwa huru katika siku za usoni.

Agizo la Rais Ashraf Ghani la kuachiwa huru wanachama wa Taliban linapaswa kutathminiwa kwa kina hasa kwa kuzingatia msimamo wa hapo kabla wa Rais huyo kuhusiana na kadhia hiyo.

Baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati ya Marekani na wanamgambo wa Taliban katika mji mkuu wa Qatar, Doha, Ashraf Ghani alisema kuwa, uamuzi kuhusiana na kuachiliwa huru wanachama wa kundi hilo utafanyika katika mchakato wa mazungumzo baina ya Waafghani na kwamba, serikali ya Washington haina ustahiki wa kuchukua maamuzi yoyote katika uwanja huo.

Katika makubaliano yake na Taliban, serikali ya Marekani iliahidi katika moja ya vipengee vya makubaliano hayo kwamba, baada ya kutiwa saini makubaliano hayo wafungwa 5,000 wa kundi hilo wataachiliwa huru. Kutokana na kuwa, huo ni uingiliaji wa wazi wa Marekani katika masuala ya ndani ya Afghanistan, jambo hilo lilikabiliwa na radiamali kali ya viongozi wa Kabul na duru za habari za nchi hiyo.

Wanamgambo wa Taliban nao kwa kutegemea ahadi hiyo, katika siku za hivi karibuni mara kadhaa wametoa wito wa kuachiliwa huru wanachama wake kabla ya kuanza mazungumzo baina ya Waafghani.

3470888

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: