IQNA

Rais Hassan Rouhani
22:37 - March 26, 2020
News ID: 3472604
TEHRAN (IQNA)- Rais Hassan Rouhani wa Iran ametangaza mipango na mikakati mipya ya kudhibiti maambukizi ya kirusi cha corona hapa nchini ndani ya wiki mbili zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa, Rais Rouhani amemuandikia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, akimuomba ridhaa ya serikali kutoa dola bilioni moja kutoka kwenye Hazina ya Taifa ya Maendeleo, zitakazotumika katika jitihada za kupambana na ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na kirusi cha corona.

Huku akipongeza hatua ya Vikosi vya Ulinzi ya kutayarisha vitanda 4,000 vya dharura, Dakta Rouhani amesema, "katika hali ambayo mataifa mengine duniani yanakabiliwa na wakati mgumu kukabiliana na mlipuko wa corona, lakini hapa nchini tuna vitanda vitupu 20,000 katika hospitali zetu."

Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, licha ya kuwa taifa hili lipo chini ya vikwazo, lakini limejitosheleza kwa chakula na mahitaji mengine ya msingi, ikilinganishwa na hata nchi nyingi zilizostawi.

Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Afya ya Iran, Kianoush Jahanpour amesema leo Alkhamisi kuwa, hadi kufikia sasa watu 10,457 waliokuwa wameambukizwa kirusi cha corona nchini Iran wamepata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitali.

Ameongeza kuwa, wagonjwa 157 wa ugonjwa wa COVID-19 maarufu kama corona wamefariki dunia ndani ya saa 24 iliyopita na kuifanya idadi ya watu wote waliopoteza maisha kutokana na maambukizo ya kirusi hicho hapa nchini kufikia 2,234. Jahanpour ameongeza kuwa, hadi sasa zaidi ya watu milioni 50 wamepimwa kupitia mpango wa uhamasishaji wa kitaifa wa kukabiliana na corona nchini Iran.

3887323

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: