IQNA

Rais wa Iran katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Japan

Hakuna njia nyingine ya kukabiliana kwa mafanikio na corona isipokuwa kushirikiana nchi zote

19:25 - May 05, 2020
Habari ID: 3472737
TEHRAN (IQNA)- Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Hakuna njia nyingine ya kukabiliana kwa mafanikio na corona isipokuwa kushirikiana nchi zote"

Rais Rouhani ameyasema hayo Jumanne katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Japan Abe Shinzo ambapo ameishukuru serikali ya Japan kutokana na misaada yake kwa Iran katika kukabiliana na janga la corona. Rais Rouhani amesema Marekani imeshadidisha vikwazo dhidi ya Iran katika kipindi hiki kigumu cha kukabiliana na corona na halikadhalika hali ngumu ya kiuchumi iliyotokana na ugojwa huo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu madai ya Marekani kuwa iko tayari kuisadia Iran kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 (corona) na kusema: "Iwapo Wamarekani ni wakweli, njia pekee ni kuondoa vikwazo vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya Iran."

Ameongeza kuwa: "Serikali ya Iran imekumbwa na matatizo makubwa katika kujidhaminia vifaa vya kitiba na vyakula kutokana na kushadidishwa vikwazo vya kidhalimu na vilivyo dhidi ya ubinadamu vya Marekani."

Rais wa Iran aidha amesisitiza kuhusu udharura wa kuendelezwa jitihada za kupunguza taharuki katika eneo la Asia Magharibi na dunia na kuongeza kuwa: "Hatua za Marekani katika wiki za hivi karibuni zimepelekea kushadidi taharuki nchini Iraq na eneo la Ghuba ya Uajemi.

Waziri Mkuu wa Japan naye kwa upande wake amesisitiza kuhusu udharura wa kushirikiana nchi zote ili kuweza kuvuka kwa mafanikio kipindi hiki kigumu cha janga la corona na mgogoro wa kiuchumi duniani ambao umetokana na janga hilo. Amesisitiza kuwa, katika hali kama hii ya sasa duniani, kuongezeka taharuki katika eneo la Asia Magharibi ni jambo linaloibua wasiwasi mkubwa.

Abe Shinzo ameitaja Iran kuwa nchi muhimu na yenye taathira katika kuleta amani na utulivu katika enei na kuongeza kuwa, Tokyo iko tayari kushirkiana na Tehran katika uga huo.

3896726

captcha