Akizungumza Jumapili katika kikao cha Idara ya Kitaifa ya Kupambana na Corona, Rais Rouhani amesema imeamuliwa misikiti ifunguliwe katika maeneo 132 kuanzia Jumatatu.
Aidha alisisitiza kuwa kanuni zote za kiafya za kuzuia corona zinapaswa kuzingatia katika misikiti na maeneo ya ibada.
Halikadhalika Rais Rouhani amesema sala ya Ijumaa itaswaliwa katika maeneo hayo. Iran ilitangaza kufunga misikiti na maeneo ya ibada mwezi Machi kuzuia kuenea corona.
Kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa waumini watakaofika misikitini watalazimika kuvaa maski na muda wa kusalia msikitini wakati wa ibada hautazidi nusu saa
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amezungumzia pia mafanikio yaliyopatikana ya kufanyiwa uchunguzi wa corona watu milioni 78 nchini Iran katika hatua ya awali ya mpango wa taifa zima wa kupambana na COVID-19 na kuongeza kuwa, katika awamu ya pili pia watu milioni 30 wameshashirikishwa kwenye zoezi hilo na kwamba awamu hii ya pili inafanyika kwa kina zaidi na kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Aidha amewashukuru wananchi kwa kufuata maelekezo ya maafisa wa afya kiasi kwamba kiujumla asilimia 83 ya watu wamefuata maelekezo hayo huku baadhi ya miji ni asilimia 92 ya walioheshimu maagizo hayo.
Vile vile amesema, katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, watu waliokwenda mahospitalini kwa ugonjwa wa corona wamepungua sana nchini Iran na wamekaribia watu 300.
Wakati huo huo Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi kufikia Mei 3 waathiriwa 78 elfu na 422 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata nafuu na afya njema na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran alitangaza hayo katika kikao cha kila siku na waandishi habari na huku akigusia kugunduliwa watu wapya 976 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha masaa 24 nchini Iran amesema, hadi kufikia jana adhuhuri watu 97,424 walikuwa wamethibitishwa kupata ugonjwa wa corona humu nchini.
Daktari Jahanpur hali kadhalika ameashiria kufariki dunia wagonjwa 47 wa corona nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia jana adhuhuri na kusema kuwa, hadi hivi sasa watu 6,203 wameshafariki dunia kwa COVID-19 humu nchini.