IQNA

Katika Barua ya Nchi 8 kwa Katibu Mkuu wa UN

Vikwazo vina athari mbaya katika vita dhidi ya corona

22:49 - March 26, 2020
Habari ID: 3472605
TEHRAN (IQNA)- Iran, Russia, China, Cuba, Korea Kaskazini, Iraq, Venezuela na Nicaragua zimemuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo mbali na kusisitiza kuwa ugonjwa wa COVID-19 aucorona ni adui wa pamoja wa nchi zote, zimetahadharisha kwamba, vikwazo vina taathira hasi na mbaya kwa udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa huo.

Katika barua yao hiyo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, wawakilishi wa nchi hizo nane katika umoja huo wamebainisha kuwa, hatua za utumiaji nguvu na za upande mmoja, zisizo za kisheria na zenye kukiuka waziwazi sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa ambazo zinachukuliwa dhidi ya nchi kadhaa hivi sasa, zinatatiza na kukwamisha juhudi za nchi hizo za kukabiliana na janga la corona.

Ikiashiria ripoti ya wataalamu wa kujitegemea wa Umoja wa Mataifa inayoeleza kwamba, utumizi wa hatua za nguvu za upande mmoja unaiathiri theluthi nzima ya jamii ya wanadamu barua hiyo imesisitiza kwamba: Haifai kuruhusu malengo na matashi ya kisiasa yakwamishe juhudi za kuokoa maisha ya watu.

Sehemu nyingine ya barua hiyo ya wawakilishi wa nchi nane wanachama wa Umoja wa Mataifa imekumbusha kuwa, kukabiliana na janga la corona kunahitaji mshikamano, ushirikiano na nchi kusaidiana kwa kiwango cha juu kabisa na ikasisitiza kwamba, uwekaji vikwazo unadhoofisha jitihada mtawalia zinazofanywa na serikali za mataifa kwa ajili ya kupambana na corona hususan katika uandaaji athirifu na kwa wakati wa zana na vifaa vya utabibu vikiwemo vifaa vya kupimia na dawa zinazohitajika kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa.

Aidha wawakilishi wa Iran, Russia, China, Cuba, Korea Kaskazini, Iraq, Venezuela na Nicaragua katika Umoja wa Mataifa wamemtaka Katibu Mkuu wa umoja huo ahakikishe, vikwazo hivyo haramu, vya uchukuaji hatua bila kujali na vyenye kutoa mbinyo na mashinikizo ya kiuchumi, vinaondolewa kikamilifu na kwa haraka.

3887476

captcha