IQNA

Fatwa ya kuruhusu misikiti kutumika kuwatibu wagonjwa wa corona

13:33 - April 12, 2020
Habari ID: 3472660
TEHRAN (IQNA)- Sheikh Ali Mohiuddin Al-Qaradaghi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa Maulamaa wa Waislamu (IUMS) ametoa fatwa ya kuruhusu kutengwa maeneo maalumu misikitini kwa ajili ya kuwatibu watu ambao wanaugua ugonjwa wa corona au COVID-19.

Sheikh Al Qaradaghi amenukuliwa na televisheni ya Al Jazeera akisema: "Fatwa hii ni katika kuhuisha Sunna ya Mtume SAW na kusisitiza kuhusu namna Uislamu unavyozingatia maisha ya mwanadamu."

Ametoa mfano na kusema wagonjwa na waliojeruhiwa walikuwa wakitibiwa katika Al-Masjid an-Nabawi mjini Madina wakati wa zama za Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW ambapo mtukufu huyo aliweka hema ndani ya Msikiti kwa ajili ya kumtibu Sa'd ibn Mu'adh alipojeruhiwa katika vita vya Khandaq. Sheikh Al Qaradaghi amesema kwa kuzingatia nukta hiyo wagonjwa wa COVID-19 wanaweza kutibiwa katika eneo maalumu ndani ya msikiti.

Msomi huyo wa Kiislamu amesisitiza kuwa hadhi ya msikiti inapaswa kulindwa wakati wa kutumiwa kama eneo la matibabu. Ameongeza kuwa ingawa misikiti imefungwa kutokana na kuenea corona lakini madaktari na wafanyakazi wa sekta za afya wanaweza kuswali katika misikiti kwa kuzingatia kanuni za kiafya na kwa baraka zake inaweza kutumika katika kupunguza machungu ya wagonjwa sambamba na kuondoa mzigo katika hospitali za serikali.

Aidha amesema hatua kama hivyo itaonyesha taswira nzuri ya Uislamu na kwamba misikiti ya Waislamu ina nafasi muhimu katika kupunguza masaibu ya wagonjwa na kuleta utulivu wa kiroho kwa wagonjwa hasa kutokana na sauti nzuri ya Qur'ani.

Sheikh Al Qaradaghi amesema utakelezwaji wa Fatwa hii utategemea kuafikiwa na wasimamizi wa misikiti na taasisi husika za kiafya.

3890999

captcha