“Maneno ni amana, na kutoa Fatwa ni jukumu kubwa. Kulinda ulimi ni jambo la lazima,” alisema Duwaidar wakati wa uzinduzi wa mafunzo kwa waandishi wa habari katika Dar al-Ifta, taasisi rasmi ya utoaji wa fatwa nchini Misri.
Alisisitiza kuwa Misri iko karibu kutekeleza sheria ya kuandaa utoaji wa fatwa, hatua muhimu katika kukabiliana na maamuzi ya kidini yasiyo na udhibiti rasmi.
Duwaidar alisifu juhudi hizo kuwa ni “hatua muhimu ya kufikisha ujumbe wa Uislamu na kukuza uelewa wa Kiislamu.” Aidha, alihimiza ushirikiano wa karibu zaidi kati ya taasisi za kidini na vyombo vya habari ili kueneza haki duniani.
Bunge la Misri limekamilisha sheria ya “Usimamizi wa Fatwa za Kidini”, ambayo inaweka mfumo wa kisheria wa kusimamia utoaji wa fatwa nchini humo. Sheria hii imekuja kufuatia ongezeko la fatwa zisizo rasmi ambazo zimezua mijadala mikali katika jamii ya Wamisri.
Ingawa sheria hiyo imeungwa mkono na Al-Azhar, Wizara ya Awqaf, na Dar al-Ifta, baadhi ya makundi, hasa Chama cha Waandishi wa Habari, wameeleza wasiwasi kuhusu vipengele vinavyoweza kutishia uhuru wa vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, ni taasisi zilizoidhinishwa pekee, kama vile Baraza la Maulamaa Wakuu, Taasisi ya Utafiti wa Kiislamu ya Al-Azhar, na Dar al-Ifta, ndizo zitakazoruhusiwa kutoa fatwa za umma zinazogusa jamii kwa ujumla.
Fatwa binafsi, zinazohusu mtu mmoja mmoja, lazima zitolewe na kamati maalum chini ya Wizara ya Wakfu, kwa sharti kwamba zinakidhi vigezo vya kitaaluma vya Al-Azhar.
Vyombo vya habari vimepigwa marufuku kuchapisha fatwa ambazo hazijatolewa na taasisi hizo rasmi. Wanaokiuka masharti hayo watakabiliwa na adhabu, ikiwemo kifungo cha hadi miezi sita na faini ya hadi pauni 100,000 za Kimisri.
Serikali imeitetea sheria hiyo kama “hitaji la kitaifa na kidini” kwa lengo la kuleta nidhamu katika utoaji wa fatwa. Sheria hiyo pia inaweka masharti makali kwa wale wanaotaka kuwa ma-mufti, ili kuzuia maamuzi ya kidini yanayopotosha au yenye misimamo mikali.
3493850