IQNA

Maulamaa UAE watoa Fatwa kuhusu saumu katika wakati wa janga la corona

23:22 - April 20, 2020
Habari ID: 3472684
TEHRAN (IQNA) – Baraza la Fatwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) limetoa Fatwa kuhusu Saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wakati wa janga la corona au COVID-19.

Katika kikao chao kwa njia ya video, maulamaa wanachama wa baraza hilo wamesema Saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni wajibu kwa Waislamu wote wenye uwezo wa kimwili.

Aidha wanazuoni hao wa UAE wamesema wale wenye dalili za ugonjwa wa COVID-19 wanaruhusiwa kutofunga Saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Halikadhalika wameongeza kuwa: “Iwapo daktari atamshauri mtu kutofunga kwa sababu saumu itaathiri kinga yake ya mwili, basi hanaweza kutofunga Saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.” Pia wanazuoni hao wa Kiislamu nchini UAE wamesema wafanyakazi wa sekta ya afya wana haki ya kuamua iwapo watafunga au la.

Katika Fatwa nyingine, Baraza la Fatwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu limesema Mwislamu anaweza kuswali Sala ya Taraweh ndani ya nyumba ima furada yaani peke yake au katika jamaa ya watu walio ndani ya nyumba. Halikadhalika wanazuoni hao wanasema inaruhusiwa kusoma Qur’ani ukiwa umeishika mkononi wakati wa Swala.

Aidha  Baraza la Fatwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu limetoa Fatwa ya kuruhusu Swala wa Idi kuswaliwa majumbani kwa kuzingatia kuwa mijumuiko imepigwa marufuku.  Hatahivyo wamesema Sala ya Ijumaa haiwezi kuswaliwa majumbani na badala yake Waislamu wanapaswa kuswali Sala ya Adhuhuri.

Halikadhalika wanazuoni hao wa Kiislamu nchini UAE wameshauri kuwa, Zakati na Zakat ul Fitri zinaweza kutolewa mapema kwa kuzingatia hali ya sasa ili kuwasaidia watu walio katika hali ngumu.

Serikali ya UAE imepiga marufuku mijumuiko yote ya Umma na kutangaza kuwa  swala za jamaa zimesitishwa kwa muda katika misikiti ya nchi hiyo ili kuzuia kuenea ugonjwa hatari wa COVID-19.  Aidha UAE imefunga shule, vyuo vikuu, maeneo ya kibiashara na kusitisha safari zote za ndege za kimataifa nchini humo kutokana na corona.

Hadi  kufikia Aprili 21, watu 7,265 wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19 nchini UAE huku 43 wakiwa wamepoteza maisha.

3892817

captcha