IQNA

WHO yatahadharisha kuhusu kuenea COVID-19 barani Afrika

0:08 - April 18, 2020
Habari ID: 3472676
TEHRAN (IQNA)- Shirika la Afya Duniani (WHO) katika Kanda ya Afrika limetahadharisa kuwa kesi za maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 au corona barani Afrika zinaweza kuongezeka kutoka maelfu ya sasa na kufikia milioni kumi katika kipindi cha miezi sita.

Daktari  Michael Yao mkuu wa oparesheni za dharura katika Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika ametoa kauli hiyo na kuongeza kuwa, kuwa ni vigumu kwa sasa kutoa makadirio ya muda mrefu kwa sababu hali ya mambo inabadilika sana, na iwapo hatua za afya katika jamii zitatekelezwa kikamilifu jambo hilo linaweza kuwa na taathira.

Bara la Afrika hadi sasa limethibitisha jumla ya kesi zaidi ya 18,400 za maambukizi ya Covid-19 na vifo karibu 1000 kufikia Aprili 17. Hata hivyo kuna wasiwasi kwamba idadi ya vifo inaweza kupanda na hivyo kulemaza sekta dhaifu za afya za nchi za bara hilo.  

Afrika Kusini kesi zapungua

Naye Daktari Matshidiso Moeti Mkurugenzi wa WHO katika Kanda ya Afrika unaojumuisha nchi 46 zilizo chini ya Jangwa la Sahara amesema kuwa kuna wasiwasi kwamba virusi vya corona vitaendelea kuenea kijiografia baina ya nchi mbalimbali.

Bi Moeti ameongeza kuwa, maambukizi ya virusi vya corona nchini Afrika Kusini ambayo ilikuwa na idadi kubwa ya kesi za virusi hivyo sasa yameanza kupungua  baada ya kuchukuliwa hatua kali za kuzuia maambukizi nchini.  

Aidha ametahadharisha kuwa hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kulikatia Shirika la Afya Duniani vyanzo vya fedha inaweza kuathiri mapambano dhidi ya virusi vya corona na kukwamisha vita dhidi ya maradhi mengine kama polio, HIV na malaria barani Afrika.

WHO yatahadharisha kuhusu kuenea COVID-19 barani Afrika

Tanzania maambukizi yaongezeka ghafla

Wakati huo huo, idadi ya kesi za wagonjwa wa Covid 19 nchini Tanzania imeongezeka na kufikia kesi 147 hadi kufikia Aprili 17, baada ya wagonjwa wengine wapya 53 kukutwa na virusi vya Corona hii leo.

Akitoa taarifa hiyo, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Ummy Mwalimu amesema kuwa, wagonjwa hao wote ni Watanzania ambapo 38 ni kutoka mkoa wa Dar es Salaam, Zanzibar wagonjwa 10, Kilimanjaro mgonjwa mmoja, Mwanza mgonjwa mmoja, Pwani mgonjwa mmoja, Lindi mgonjwa mmoja na Kagera mgonjwa mmoja.

Wakati huo huo, Kenya imetangaza kuwa, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona nchini humo hadi kufikia Aprili 17 ni 246.

Uganda hakuna ongezeko

Nchini Uganda takwimu za wizara ya afya zinaonyesha kuwa, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona nchini humo imeendelea kubakia 55 kwa siku kadhaa huku 20 kati yao wakipona na kwamba, hadi sasa hakuna mtu aliyefariki kwa ugonjwa huo.

Burundi kwa upande wake imesajili kesi tano za maambukizi ya virusi vya Corona na kifo kimoja hadi sasa, huku jirani yake Rwanda ikithibitisha kesi 138 za maambukizo na 60 kati yao wakipona na kutoripotiwa kifo cha Corona nchini humo hadi sasa.

3892218

captcha