IQNA

Corona Afrika Mashariki na Kati

Kenya na Somalia zaachilia wafungwa, mtaa wa Gombe Kinshasa katika karantini

21:28 - April 03, 2020
Habari ID: 3472630
TEHRAN (IQNA)- Huku ugonjwa wa corona au COVID-19 ukiendelea kuenea barani Afrika, nchi za bara hilo zinachukua hatua za kuzuia maambukizi zaidi.

Kenya na Somalia zimetangaza kuwaachilia huru wafungwa wa makosa madogo madogo ikiwa ni katika jitihada za kupunguza msongamano katika magereza katika kipindi hiki cha kuenea ugonjwa hatari wa corona au COVID-19.

Wafungwa Kenya waachiliwa

Siku ya  Alhamisi Kenya ilitangaza kuwaachilia huru wafungwa  3,837 ili kuzuia kuenea ugonjwa wa COVID-19 katika magereza. Taaarifa ya Idara ya Magereza Kenya imesema uamuzi huu unalenga kuhakikisha kuwa kila mtu anakaa umbali wa mita moja na mwenzake kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa kimataifa katika vita dhidi ya janga la COVID-19.

Aidha Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga ameamuru kuwa wanaofanya makossa madogo madogo na makossa ya trafiki wasikae katika seli za vituo vya polisi kwa zaidi ya masaa 24.  Kwa upande wake, Rais wa Somalia ametoa msamaha kwa wafungwa 148 ikiwa ni juhudi za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Rais wa Somalia awasamehe wafungwa

Rais Mohamed Farmajo wa Somalia, ametoa msamaha kwa wafungwa 148 ikiwa ni sehemu ya hatua za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona nchini humo.

Mpaka sasa, kesi zilizothibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona nchini Somalia zimefikia tano, zikiwa ni raia watatu wa Somalia na raia wawili wa kigeni.

Hadi sasa watu 110 wameambukizwa corona nchini Kenya na miongoni mwao watatu wamefariki.

Karantini mjini Kinshasa

Wakati huo huo Serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuzuia watu kutoka au kuingia katika wilaya ya Gombe katika mji mkuu, Kinshasa.

Uamuzi huo wa karantini ya eneo hilo umechukuliwa baada ya kubainika kuwa wilaya ya Gombe ni kitovu cha ugonjwa wa corona au COVID-19.

Hadi sasa watu  134 wamethbitishwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 nchini DRC na miongoni mwao 13 wamefariki dunia. Ugonjwa huo umeripotiwa katika mikoa mitatu ikiwa ni pamoja na mji mkuu Kinshasa.

Wiki iliyopita Gavana wa Mkoa wa Kinshasa alitangaza sheria ya  kutotoka nje kwa wakazi wa mkoa huo kabla ya kubatilisha uamuzi wake.

Gavana wa Mkoa wa Kinshasa, Gentiny Ngobila, amehakikisha kwamba hatua hiyo imechukuliwa baada ya mamalaka zote nchini humo kufikia makubaliano.

Kwa muda wa wiki mbili hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingia au kutoka katika Wilaya ya Gombe isipokuwa tu wafanyakazi wa afya na waandishi wa habari.

Vifo Afrika

Hadi sasa watu 7,064 wameambukizwa corona kote Afrika huku wengine 290 wakipoteza maisha lakini waledi wa mambo wanaamini kuwa yamkini idadi huwa ikawa juu zaidi.

3888762

Kishikizo: Corona kenya afrika
captcha