IQNA

Rais wa Afrika Kusini awatumia Waislamu Salamu za Ramadhani

10:29 - April 26, 2020
Habari ID: 3472705
TEHRAN (IQNA) - Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amewatumia Waislamu salamu kwa mnasba wa kuwadia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Katika ujumbe huo Ramaphosa amesema: “Hilali ya mwezi imeonekana katika bara letu la Afrika na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umeanza. Kwa niaba ya Umoja wa Afrika, nawatakia Waislamu kila la kheri katika mwezi huu.”

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ametoa wito kwa Waislamu kuzingatia kanuni ambazo zimewekwa ili kukabiliana na corona katika mwezi huu mtukufu. Amesema nchi kadhaa zimeweka sheria za kuzuia corona na hilo lina maana kuwa, kinyume na ilivyo ada katika mwezi wa Ramadhani, Waislamu hawataweza kuswali misikitini, kutembelea familia na marafiki na pia hawataweza kutekeleza ibada ya Umrah.

Mwenyekiti  wa Umoja wa Afrika amesema kama tunataka kupata ushindi katika makabiliano na janga la corona, kuna haja ya kuwa na umoja na kuzingatia kanuni za afya zilizowekwa ili tulinde afya zetu na za wengine.

Hadi sasa kuna kesi 27,385 za corona au COVID-19 barani Afrika huku watu 1,297 wakiwa wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo.

Ramaphosa pia ametoa wito kwa Waislamu kuendelea na ukarimu wao wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuwasaidia wasiojiweza katika jamii katika kipindi hiki ambacho mamilioni wamekumbwa na njaa.

/3471254

captcha