IQNA

Indhari ya Jordan kuhusu hatari ya mapigano iwapo Israel itateka maeneo ya Ukingo wa Magharibi

8:52 - May 17, 2020
Habari ID: 3472774
TEHRAN (IQNA) - Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan ameutahadharisha utawala wa Israel kuwa utaraji mapigano makubwa iwapo utasonga mbele na mpango wake wa kuteka zaidi ardhi za Palestina katika Ukingo wa Magharibi na Bonde la Jordan.

Mfalme Abdullah ameyasema hayo katika mahojiano yake na jarida la Der Spiegel na kuongeza kuwa nchi yake inatafakari kuhusu machaguo yoyote katika kukabiliana na mpango wa utawala  wa Israel wa kuanza kuteka zaidi ardhi za Palestina mwezi Julai.

Aidha ameashiria kuwa Jordan inaweza kuamua kusitisha mapatano tata ya amani baina yake na Israel.

Matamshi hayo yamekuja baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kupokea idhini ya serikali mpya ya mseto kuhusu kupigiwa kura mpango wake wa kuteka ardhi zaidi za Palestina.

Mpango huo unaungwa mkono kikamilifu na Marekani na umekuwa ukikosolewa vikali kwani Israel inalenga kuziteka na kuzifanya kuwa milki yake ardhi ambazo ilizikalia kwa mabavu mwaka 1967 baada ya vita na Waarabu.

Kwa mtazamo wa jamii ya kimataifa, eneo lote la Ukingo wa Magharibi na upande wa mashariki wa mji wa Quds (Jerusalem) ni ardhi ambazo zinapaswa kuwa sehemu ya taifa huru la Palestina katika mustakabali.

3899386

captcha