IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasita hata kidogo kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina

21:33 - July 06, 2020
Habari ID: 3472933
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasita hata kidogo katika kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na kuvunja shari za utawala bandia na ghasibu wa Kizayuni.

Ayatullah Khamenei ametoa sisitizo hilo katika barua yake ya majibu kwa barua ya mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas kuhusiana na matukio ya hivi karibuni ya Palestina.

Katika barua yake hiyo kwa Ismail Haniya, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Kiongozi Muadhamu amesifu na kupongeza hatua za muqawama wa Palestina, katika kukabiliana na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni, ambazo zimeupa izza na heshima umma wa Kiislamu; na akabainisha kwamba: "Adui dhalili ambaye amepata vipigo visivyoweza kufidika katika medani ya mapambano, anaendeleza mkakati wake wa kujipanua na kupora haki zisizo na shaka za Wapalestina, aliouanzisha kwanza kwa mashinikizo ya kiuchumi na mzingiro dhidi ya Gaza inayodhulumiwa, na kisha akauendeleza kwa hila na ghilba ya mazungumzo na mpango wa suluhu na mapatano."

Katika barua hiyo iliyotangazwa katika vyombo vya habari leo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kwa kutumia mantiki ya akili na tajiriba, vuguvugu la mapambano au muqawama na taifa shujaa la Palestina halitaghilibiwa na vitisho na vivutio vya maadui; na kama ilivyokuwa huko nyuma wakati liliposhikamana na njia yake ya izza na heshima kwa kusimama imara kwa kiwango cha kupigiwa mfano, hivi sasa litaendelea kushikamana na kufuata njia yake iliyonyooka.

Katika sehemu nyingine ya barua yake hiyo kwa kiongozi wa Hamas, Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kuhusu udharura wa kuwa macho na kudumishwa umoja na mshikamano wa wananchi na harakati za Palestina ili kuzima njama chafu za adui; na akakumbusha kuwa: Kama ilivyokuwa huko nyuma na kwa kuzingatia wajibu wake wa kidini na kiutu na uliosimama juu ya misingi ya thamani za Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasita kufanya kila jitihada kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina, kupigania kupatikana haki zao na vilevile kuvunja na kuzima shari ya utawala bandia na ghasibu wa Kizayuni.

3908995

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha