IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

UAE imeusaliti Ulimwengu wa Kiislamu na Palestina, hali hii haitadumu

20:40 - September 01, 2020
Habari ID: 3473127
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja hatua ya serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni kuwa ni kuusaliti Ulimwengu wa Kiislamu, Ulimwengu wa Kiarabu na nchi za eneo na kadhia muhimu ya Palestina.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameashiria kuanzishwa uhusiano kati ya Imarati na utawala wa Kizayuni na kueleza kuwa: hali hii haitadumu hata hivyo doa la fedheha litabaki katika vipaji vya uso vya wale wote wanaosahaulisha kughusubiwa nchi ya Palestina na kuwafanya Wapalestina kuwa wakimbizi na kutoa mwanya wa kujipenyeza Wazayuni katika eneo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo asubuhi mjini Tehran wakati akihutubia kwa njia ya intaneti kikao cha 34 cha Elimu na Malezi Iran kilichohudhuriwa na Waziri, Manaibu, Wakurugenzi na Maafisa wa Wizara ya Elimu na Malezi ya Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kusikitishwa na ushirikiano wa serikali ya Imarati kwa vitendo vya kikatili vya utawala wa Kizayuni na vibaraka waovu wa Kizayuni katika serikali ya Marekani dhidi ya maslahi ya Ulimwengu wa Kiislamu na eneo na kueleza kuwa: anataraji kuwa Waimarati wataamka na kuwa macho haraka iwezekenavyo na kufidia hatua yao hiyo. 

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameashiria sisitizo la Wamagharibi la kujipenyeza katika mfumo wa elimu na malezi wa nchi nyingine kwa lengo la kuzitwishwa mfumo wao wa maisha  kupitia hati ya 2030 au kujipenyeza katika mifumo ya elimu na malezi ya baadhi ya nchi za eneo na kueleza kuwa: leo hii falsafa ya kijamii ya Magharibi imefeli huko huko Magharibi na taathira za ufisadi wake huo zinadhihirika kikamilifu kuanzia Hollywood hadi Pentagon. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameyataja maombolezo ya taifa la Iran katika siku kumi za mwanzo za mwezi wa Muharram mwaka huu kuwa ya aina yake katika historia na kuongeza kuwa, “kwa kuzingatia kanuni na miongozo mikali iliyowekwa kutokana na maambukizi ya corona; wananchi waombolezaji na watoa mihadhara walifuata miongozo hiyo kwa kudumisha hamasa ya Imam Hussein AS  na kuendesha majlisi adhimu na za kimaanawi; na mimi, nikiwa mfuasi wa Ahlul Bait ninatoa shukurani zangu za dhati kwa wapendwa wote.”

3920299

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :