IQNA

Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa Waislamu

Ni haramu kuwa na uhusiano na utawala wa Israel

13:08 - September 01, 2020
Habari ID: 3473125
TEHRAN (IQNA) - Mkuu wa Umoja wa Kimataifa wa Maulamaa wa Kiislamu amesema kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, ni haramu kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika hotuba na jarida la al-Shuruq la Algeria, Sheikh Ahmed al-Raissouni amelaani hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema hatua hiyo itaupa kiburi zaidi utawala huo kuendeleza jinai dhidi ya Wapalestina.

Ameongeza kitendo cha baadhi ya nchi za Kiarabu cha kuweka uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kufumbia macho jinai za utawala huo katili dhidi ya wananchi wa Palestina.

Sheikh al-Raissouni ameongeza kwamba, kitendo cha baadhi ya nchi za Kiarabu zikiwemo Imarati na Saudi Arabia cha kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kutoa huduma ya bure kwa utawala huo na ni katika juhudi za kuiokoa Israel kutoka katika kinamasi kikubwa ilichokwama.

Amesema, kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ni sawa na kuunga mkono kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina na ni kama vile kuwapa zawadi viongozi wa Israel kutokana na jinai zao zisizo na kifani wanazowafanyia Wapalestina.

Rais wa Marekani, Donald Trump amekuwa akifanya njama za kila namna za kuhakikisha nchi za Kiarabu zinakuwa na uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Israel. Siku ya Alkhamisi ya tarehe 13 Agosti, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na utawala wa Kizayuni zilifikia makubaliano ya kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia baina yao.

Si hayo tu, lakini vile vile viongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu wameanzisha pia safari za moja kwa moja za ndege baina yake na utawala wa Kizayuni na ndege ya kwanza ya shirika la El Al la utawala bandia wa  Israel ilitua jana Jumatatu katika uwanja wa ndege wa Abu Dhabi nchini UAE.

3472426

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :