IQNA

Qatar, Pakistan zasema hazitaanzisha uhusiano na utawala wa Israel

21:28 - September 15, 2020
Habari ID: 3473172
TEHRAN (IQNA) – Qatar imesema katu haitafuata nyao za majirani zake yaani tawala za Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambazo zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Lolwah Rashid al-Khater ameiambia televisheni ya Bloomberg kuwa nchi yake haiamini kuwa uanzishwaji uhusiano wa kawaida na Israel ni suluhisho kwa mgogoro wa Palestina. Amesema kiini cha mgogoro huo ni hali mbaya ya kimaisha ya Wapalestina ambao wanaishi kama watu wasio na nchi na ambao ardhi zao zimekaliwa kwa mabavu.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amesema nchi yake haitalegeza msimamo kuhusu kadhia ya Palestina. Amesema kuutambua utawala wa Israel ni jambo ambalo litapingwa vikali na watu wa Palestina na kuongeza kuwa uamuzi kama huo unaenda kinyume cha matakwa ya taifa linalodhulumiwa la Palestina. Amesema hata dunia nzima ikiitambua Israel, Pakistan haitachukua uamuzi kama huo.

UAE na Bahrain leo Jumanne zinatarajiwa kutia saini mapatano eti ya amani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika ikulu ya Rais wa Marekani, White House, mjini Washington. Hatua hii imeyakasirisha sana mataifa ya Waislamu na Waarabu ambayo yameitaja kuwa ni usaliti dhidi ya Uislamu, Palestina na Quds tukufu.

Mapatano hayo yalitazamiwa kusainiwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Imarati,Bahrain na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. 

Kuhusiana na kadhia hiyo Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh amesema: "Leo Jumanne ni siku nyeusi katika historia ya uliwengu wa Kiarabu na siku ya kufeli Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League). Jumuiya hii sasa ni taasisi ya kuzusha migawanyiko na si jumuiya ya Waarabu. Hii itakuwa tarehe nyingine ya kuongezea katika kalenda ya matukio chungu ya Palestina."

Malalamiko na upinzani dhidi ya hatua hiyo ya Imarati na Bahrain ya kuanzisha uhusiano na utawala katili unaoendelea kuua Wapalestina havikuishia katika ngazi ya wanasiasa wa Palestina bali umepanuka zaidi hadi kwenye makundi na harakati za kupigania ukombozi za Palestina na makundi ya wananchi na watetezi wa haki za binadamu na za kiraia katika nchi mbalimbali za Kiislamu. Harakati za mapambano za Palestina zimeitangaza siku ya leo Jumanne tarehe 15 Septemba kuwa ni Siku ya Ghadhabu dhidi ya usaliti huo na kutangaza kwamba Ijumaa ijayo itakuwa siku ya maombolezo ya kitaifa. 

3472574

captcha