IQNA

Sudan yaiambia Marekani haina mpango wa kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel

13:45 - August 26, 2020
Habari ID: 3473103
TEHRAN (IQNA) - Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok amemfahamisa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kwamba Khartoum haiwezi kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hamdok alimweleza Pompeo, aliyekuwa ziarani Khartoum siku ya Jumanne kwamba serikali ya mpito ya Sudan ambayo ilishika hatamu baada ya kuondolewa madarakani Omar al-Bashir mwaka jana haina mamlaka ya kuchukua hatua kama hiyo. 

Sambamba na safari Pompeo mjini Khartoum maelfu ya Wasudan walifanya maandamano jana wakipinga hatua yoyote ya nchi yao kuanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel. 

Wakati huo huo, serikali ya Sudan imetoa taarifa ikiiambia Marekani kwamba suala la kuondolewa jina la Sudan katika orodha ya magaidi halipasi kushurutishwa na kunanzisha uhusiano wa kidoplomasia na utawala haramu wa Israel.

Msemaji wa Serikali ya Sudan,  Faisal Mohamed Saleh amesema katika taarifa hiyo kwamba, katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo aliyetembelea Khartoum, Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok ameitaka Washington isifungamanishe suala la kuondolewa jina la Sudan katika orodha ya magaidi na kadhia ya kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.

Hii ni baada ya duru za habari kutangaza kuwa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo anafanya safari katika nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu katika mikakati ya kuzishawishi nchi hizo zianzishe uhusiano na utawala haramu wa Israel.

Kufuatia hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kurahisisha uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)  na utawala haramu wa Kizayuni, tarehe 13 Agosti pande mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Makubaliano hayo kati ya Israel na UAE  yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani wa makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu na shakhsia kadhaa wa kisiasa duniani, ambao karibu wote wamesisitiza kwa kauli moja kuwa, hatua hiyo ya UAE ni uhaini na usaliti kwa malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina.

3472391

captcha