IQNA

Mapatano ya amani ya Sudan yakaribishwa kieneo

22:23 - September 03, 2020
Habari ID: 3473134
TEHRAN (IQNA) – Nchi za mashariki mwa Afrika zimepongeza makubaliano ya amani baina ya Serikali ya Mpito ya Sudan na Muungano wa Harakati ya Kimapinduzi kutoka jimbo la Darfur na katika majimbo ya kaskazini ili kuhitimisha mgogoro wa miaka 17 nchini humo.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, naye pia ameipongeza Serikali ya Mpito ya Sudan na Muungano wa Harakati ya Kimapinduzi kwa kufikia mapatano yao ya amani ambayo yalitiwa saini Agosti 31 huko Juba, Sudan Kusini. Faki ameyataka mapatano hayo kuwa ya Kihistoria na kusema ni ishara kuwa nchi za Kiafrika zina uwezo wa kutatua matatizo yao bila kuwepo uingiliaji wa ajinabi. Nayo Jumuiya ya Maendeleo ya Baina ya Serikali za Nchi za Mashariki mwa Afrika (IGAD)  imesema ni jambo la kupongezwa na kutia matumaini kwa pande hizo kusaini makubaliano hayo ya amani kwa ajili ya mustakabali wa wananchi wote wa Sudan.

Taarifa ya jumuiya hiyo ya kikanda imesema: Ni matumaini yetu kuwa pande ambazo hazijasaini makubaliano hayo, karibuni yataungana na ndugu zao katika jitihada hizo za kuhitimisha matatizo yanayowakabili Wasudan.

Serikali ya Sudan Kusini imekuwa ikijishughulisha kama mwenyeji na kusaidia jitihada za upatanishi katika mazungumzo yaliyokuwa yamekwama kwa muda mrefu ya Sudan tangu mwishoni mwaka 2019.

IGAD imewapongeza wadau wote waliofanikisha kufikiwa makubaliano hayo ya amani, akiwemo Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Handook, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa nchi hiyo Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na viongozi wa makundi yote yanayobeba silaha yaliyosaini mapatano hayo.

3472450

captcha