Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), shirika kubwa zaidi la kutetea haki za raia wa Kiislamu nchini humo, limelaani kitendo hicho cha ugaidi katika taarifa siku ya Jumatatu.
Kundi la kigaidi la Daesh (ISIL au ISIS) limedai kuhusika na shambulio hilo ambalo, kwa mujibu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, liliua angalau waumini 43 waliokuwa wakihudhuria ibada ya usiku katika kanisa lililoko mashariki mwa DRC.
“Mauaji ya watu katika nyumba ya ibada si kitu kingine bali ni uovu wa hali ya juu,” alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CAIR, Ibrahim Hooper. “Tunalaani shambulio hili la kinyama, na tunaomba Mungu awape faraja walionusurika na familia za waliopoteza wapendwa wao.”
Shambulio hilo lililotokea katika mji wa Komanda, jimbo la Ituri siku ya Jumapili, ambapo magaidi ADF wanaofungamana na Daesh waliwaua watu kwa kutumia bunduki na mapanga, na kuwateka wengine.
Daesh ilitangaza kupitia chaneli yao ya Telegram kuwa waasi waliwaua waumini wapatao 45 na kuchoma nyumba na maduka kadhaa.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO) ulithibitisha vifo vya watu angalau 43, wakiwemo wanawake 19 na watoto 9, na kulaani vikali kitendo hicho cha kikatili.
Papa Leo, kiongozi wa Wakatoliki duniani alituma ujumbe wa rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu na marafiki zao, akisema ataendelea kuwaombea.
Serikali ya DRC ililaani shambulio hilo la kanisani kama “tukio la kutisha,” huku jeshi likilitaja kuwa “mauaji ya kiwango kikubwa” yaliyochochewa na kisasi kufuatia operesheni za kiusalama dhidi ya ADF.
349404