IQNA

Kinara wa magaidi wa Al Qaeda tawi la kaskazini mwa Afrika aangamizwa

20:39 - November 14, 2020
Habari ID: 3473358
TEHRAN (IQNA) -Wanajeshi wa Ufaransa walioko nchini Mali wamedai kumuangamiza kinara wa operesheni za kigaidi za tawi la kaskazini mwa Afrika la mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.

Hayo yalitangazwa jana Ijumaa na Waziri wa Vikosi vya Ulinzi wa Ufaransa, Florence Parly na kuongeza kuwa, jeshi la Ufaransa limefanikiwa kumuangamiza Bah ag Moussa, katika operesheni ya Jumanne iliyojumuisha mashambulizi ya ardhini na angani.
Parly amesema, Bah ag Moussa alikuwa mtu muhimu katika harakati za kigaidi katika eneo la Sahel, na alihusika na mashambulizi mengi yaliyoua raia na maafisa usalama.

Inaarifiwa kuwa, Mousa alikuwa mtu wa karibu sana na Iyad Ag Ghali, kinara wa kundi mashuhuri zaidi la kigaidi la Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) la eneo la Sahel.

Katikati ya mwezi uliopita wa Octoba, duru za kiusalama nchini Mali zilitangaza habari ya kuuawa na kujeruhiwa makumi ya watu katika mashambulio matatu ya kigaidi. 

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaojulikana kwa jina la MINUSMA pamoja na wanajeshi wa Ufaransa, walitumwa nchini Mali tangu katikati ya mwaka 2013 lakini wameshindwa kuzuia mashambulizi ya magenge ya kigaidi.

3934929

 

captcha