IQNA

Mauaji ya Shahidi Fakhirzadeh yaendelea kulaaniwa duniani

16:35 - November 29, 2020
Habari ID: 3473405
TEHRAN (IQNA)- Nchi na viongozi mbalimbali duninani wameendelea kulaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran na kusisitiza kuchukuliwa hatua waliohusika na jinai hiyo.

Faisal Mekdad, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria amelaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na kuitaka jamii ya kimataifa itekeleze majukumu yake ipasavyo kuhusiana na vitendo vya kigaidi kama hivi.

Muhammad Bin Abdul-Rahman Al-Thani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar naye amelaani mauaji ya kigaidi ya Mohesn Fakhrizadeh mwanasayansi wa nyuklia wa Iran na kubainisha kwamba, katika hali ambayo kunafanyika juhudi za kupunguza mizozo na mivutano katika eneo la Asia Magharibi, kuuawa mwanasayansi huyu wa nyuklia kutazidi kuchochea moto wa machafuko.

Wakati huo huo, Mustafa Sentop, Spika wa Bunge la Uturuki amelaani mauaji ya mwanasayansi huyo na kuitaja hatua hiyo kuwa ni ya kigaidi.

Aidha Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Dakta Zarif na kulaani vikali mauaji hayo aliyotaja kuwa ni ya kigaidi.

Kwa upande wake, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon sambamba na kulaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran imesisitiza kuwa, iko pamoja na taifa la Iran kwa ajili ya kukabiliana na vitisho na njama za maadui.

Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran aliuawa shahidi Ijumaa iliyopita katika shambulio la kigaidi lililofanywa katika viunga vya jiji la Tehran.

Shirika la Utafiti na Ubunifu katika Wizara ya Ulinzi  ya Iran, ambalo lilikuwa likisimamiwa na Shahidi Fakhirzadeh, lilikuwa mstari wa mbele kuunda vifaa vya kupima ugonjwa wa corona. Alikuwa akiongoza jitihada za kuunda chanjo ya corona nchini na matokeo ya jitihada hizo yatatangazwa karibuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amelaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi na kuongeza kuwa, kuna dalili nzito zinazoonyesha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ulihusika katika mauaji ya Fakhirzadeh.

Katika ujumbe kupitia Twitter, Zarif ameandika: “Magaidi wamemuua mwanasayansi maarufu wa Iran leo. Kuna dalili nzito zinazoonyesha Israel imehusika na ni ishara ya wanavyotapatapa wapenda vita.”

Zarif ametoa wito kwa jamii ya kimataifa, hasa Umoja wa Ulaya kusitisha udumakuwili wenye kuaibisha na kulaani kitendo hiki cha kigaidi.

3937939

captcha