IQNA

Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Fakhrizadeh, mwanasayansi bingwa wa nyuklia Iran

20:12 - November 28, 2021
Habari ID: 3474614
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Idara ya Mahakama ya Iran amesisitiza kuwa, mauaji ya kigaidi ya wanasayansi wa nyuklia ni jinai dhidi ya binadamu na ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Kazem Gharib Abadi, ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Mhimili wa Mahakama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, mauaji ya kigaidi ya Mohsen Fakhrizadeh, kama mauaji ya mashahidi wengine wa nyuklia ni jinai dhidi ya binadamu na ni uikukaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu. 

Katika tamko alilotoa kwa mnasaba wa kuwadia mwaka mmoja tangu shahidi Fakhrizadeh alipouawa kigaidi, Gharib Abadi ameongeza kuwa, shahidi Fakhrizadeh alikuwa mwanasayansi asiyejulikana na ni baada ya kuuawa shahidi ndipo wananchi wakaweza kufahamu baadhi ya huduma muhimu sana alizotoa. Vilevile amekosoa kimya na kutochukua hatua asasi za kimataifa na nchi zinazojigamba kuwa ni wapambanaji wa ugaidi kuhusiana na jinai hiyo na akasema, mahakama ya Iran imekamilisha uchunguzi wa kisheria wa kesi nne za mauaji ya wanasayansi wa nyuklia na karibuni hivi itatoa hukumu za kesi hizo.

Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran aliuawa shahidi Novemba 28, 2020 katika shambulio la kigaidi lililofanywa kwenye viunga vya jiji la Tehran. 

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara kwa mara imekumbwa na mashambulio ya kigaidi na ya kikatili kabisa. Mauaji ya kigaidi dhidi ya shakhsia wakubwa wa kisiasa wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo kuuliwa kigaidi wananchi 17 elfu wasio na hatia ni sehemu tu ya jinai kubwa zilizofanywa na Marekani na magaidi inaowaunga mkono dhidi ya taifa la Kiislamu la Iran. Kushiriki kikamilifu Marekani katika mauaji ya kigaidi kupitia kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel kumepelekea wanasayansi kadhaa wa nyuklia wa Iran wauawe kidhulma katika miaka ya 2010, 2011 na 2012. Kumuua kigaidi Dk Mohsen Fakhizadeh, mwanasayansi mwengine mkubwa wa masuala ya nyuklia na ulinzi wa Iran ulikuwa ni muendelezo huo huo wa mauaji ya kigaidi yanayofadhiliwa na Marekani kupitia kuunga mkono kwake jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Malengo ya Kiistikbari

Hapa pana nukta kadhaa muhimu za kuzigusia kuhusu suala hilo. Mosi: Ni muundo wa kisiasa na malengo ya kiistikbari ya mashirika ya kijasusi ya Marekani na Israel na magenge yao ya kigaidi katika eneo hili na kile hasa wanachokitafuta magaidi hao. Pili: Ni njama za maadui za kujaribu kuzuia na kukwamisha maendeleo ya kielimu ya Iran hasa baada ya kuona kuwa, licha ya kwamba wanawaua kigaidi wanasayansi wa Iran, wanafanya uharibifu kwenye taasisi za nyuklia za taifa hili, wameiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha juu kabisa, lakini wameshindwa kutimiza ndoto zao. Na Tatu: Ni kujaribu kutoa pigo kwa muundo wa kiusalama na nguvu za kiulinzi za Iran. Kumuua kigaidi na kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, SEPAH, ni ushahidi wa wazi wa uhakika huo.

Undumakuwili

Kwa kweli Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kwamba siasa za nyuso mbili na za kindumilakuwili za madola ya Magharibi katika vita dhidi ya ugaidi, ndizo zilizopelekea kushindwa dunia kupambana na vitendo vya kigaidi. Tajiriba ya muongo mmoja uliopita inaonesha kuwa, kutokana na kwamba madola ya Magharibi hayako tayari kuachana na undumilakuwili wao huo, tusitarajie kabisa kupungua vitendo vya kigaidi, bali tutegemee kuongezeka kwake katika siku za usoni. 

Haki ya Iran

Noam Chomsky, mwananadharia wa masuala ya kisiasa ambaye anasema waziwazi kuwa Marekani ndiye kiranja wa ugaidi duniani, kuhusu suala hili anasema: "Maadamu Iran itaendelea kuwa nchi huru na haitokubali kuupigia magodi ubeberu wa Marekani, basi uadui wa kila namna wa Washington dhidi ya Tehran utaendelea kwani kwa mtazamo wa Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfumo usiokubalika kabisa kutokana na kuwa, hauko tayari kufumbia jicho uhuru wake."

Kwa upande wake na katika maazimio yake yote, Umoja wa Mataifa umekuwa ukisema waziwazi kuwa, vitendo vya kigaidi vinavyotokea popote pale duniani, ni uhalifu na ni jinai zisizokubalika kabisa. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo inasema wazi kuwa, ni haki yake ya dhati kuchukua hatua zozote zinazohitajika kujibu mashambulio ya kigaidi inayofanyiwa na vitendo vingine viovu vyovyote vile kwani ndivyo inavyosema hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

4016697

Kishikizo: Fakhrizadeh nyuklia iran
captcha